Dar, Bagamoyo kukumbwa na uhaba wa maji kesho

Muktasari:

Ni saa 12 kupisha matengenezo ya transifoma

Dar es Salaam. Baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam na Bagamoyo mkoani Pwani, kesho Julai 25, 2018 yatakumbwa na ukosefu wa maji baada ya mtambo wa Ruvu Chini kuzimwa.

Taarifa iliyotolewa leo na ofisa uhusiano wa Shirika la Majisafi na Maji Taka Dar es salaam (Dawasco), leo asubuhi Julai 24, 2018 imesema mtambo huo utazimwa kwa wastani wa saa 12, kuanzia saa 3:00 asubuhi mpaka saa 02:00 usiku.

Dawasco imesema kuzimwa kwa mtambo huo kunatokana na kufanya marekebisho ya transifoma.

“Dawasco inawaomba radhi wananchi wa maeneo husika kwa usumbufu utakaojitokeza, pia inawaomba kutunza maji ya kutosha kwa kipindi hicho,” imeeleza taarifa hiyo

Shirika hilo limebainisha maeneo yatakayoathirika kuwa ni; Mji wa Bagamoyo, Vijiji vya Mapinga, Icerege na Mapunga.

Maeono ya Dar es Salaam ni; Bunju, Boko, Tegeta, Kunduchi, Salasala, Jangwani, Mbezi Beach, Kawe, Mlalakuwa, Mwenge, Mikocheni, Msasani, Sinza, Manzese, Mabibo, Kijitonyama, Kinondoni, Oysterbay, Magomeni, Upanga na Kariakoo.

 

Mengine ni City Center, Ilala, Ubungo Maziwa, Kigogo, Mburahati, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Buguruni, Chang’ombe na Keko.