Dar kinara wa matusi, Mwanza wizi wa mtandaoni

Muktasari:

Ndivyo takwimu za Jeshi la Polisi zinavyoonyesha. Dar es Salaam inaongoza kwa makosa ya kutumia lugha ya matusi mtandaoni na Mwanza ni kinara wa matukio ya wizi wa mtandaoni.

Dar es Salaam. Dar es Salaam na Mwanza si tu ni majiji makubwa mawili nchini, bali pia ni makubwa kwa uhalifu wa mtandaoni; moja likiongoza kwa matusi na jingine kwa wizi.

Ndivyo takwimu za Jeshi la Polisi zinavyoonyesha. Dar es Salaam inaongoza kwa makosa ya kutumia lugha ya matusi mtandaoni na Mwanza ni kinara wa matukio ya wizi wa mtandaoni.

Takwimu za Jeshi la Polisi zinaonyesha kuwa jumla ya matukio 327 ya matusi mtandaoni yameripotiwa kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Msemaji wa jeshi hilo, Barnabas Mwakalukwa alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA).

Alisema matukio mengi ya matumizi ya lugha za matusi yanatokea wilayani Temeke.

Alipoulizwa ni mkakati gani kukabiliana na hali ya kuongoza kwa matusi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alikuwa na jibu tofauti.

“Katafute kazi nyingine na si kunihoji kwenye simu,” alisema Makonda.

Hata hivyo, takwimu hizo zinaonyesha kupungua ikilinganishwa na mwaka jana wakati matukio 911 kama hayo yaliripotiwa na wakati huo Kinondoni iliongoza kwa makosa 251.

Kuhusu wizi wa mtandaoni, jumla ya matukio 1,663 yameripotiwa na Mkoa wa Mwanza ndio unaoongoza ukifuatiwa na Wilaya ya Ilala na Kinondoni.

Mwakalukwa alisema Mwanza inaonekana kuongoza kutokana na mkoa huo kukua kwa kasi na kuwepo na wafanyabiashara wengi.

“Unaweza kuuliza kwa nini Mwanza? ule mji umekua, kuna wafanyabiashara wakubwa, wahalifu nao wanabuni mbinu mpya,” alisema.

“Kumekuwepo na dhana kuwa matukio ya uhalifu mtandaoni hayapelelezwi, niwaambie wazi si kweli. Tena hayo ndiyo rahisi kwa sababu yanaacha vielelezo vinavyosaidia polisi kufanya kazi yao,” alisema.

Mwakalukwa alisema kwa takwimu za mwaka jana, Arusha iliongoza kwa kuwa na matukio 312 ya mtandaoni ya kutishia kuua, ikifuatiwa na Kinondoni (295) na Mwanza (265).

Kwa mwaka huu, watuhumiwa 315 walikamatwa kuanzia Januari hadi Juni kutokana na uhalifu wa mtandaoni na kesi 153 zimefunguliwa mahakamani.

Kati ya kesi hizo, watuhumiwa 19 walikutwa na hatia na nyingine zipo chini ya upelelezi.

Takwimu hizo ni tofauti na za mwaka jana wakati watuhumiwa 1,080 walikamatwa kwa makosa ya uhalifu mtandaoni, huku kesi 578 zilifikishwa mahakamani na watuhumiwa katika 88 wakikutwa na hatia.