Friday, August 11, 2017

Darasa la saba aliyewania urais kupitia CCM, hakutarajia kama Dk Magufuli angeshinda

 

By Reginald Miruko, Mwananchi rmiruko@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Aliyewania nafasi ya kugombea urais kupitia CCM mwaka 2015 kwa elimu yake ya darasa la saba, Ildephonce Birohe ameibuka na kusema katika kinyang’anyiro hicho hakutarajia kama Rais John Magufuli ndiye angeibuka mshindi.

Birohe (46) alitoa kauli hiyo katika mahojiano maalumu aliyofanya na Mwananchi nyumbani kwake Mtaa wa Gezaulole, Kata ya Gungu mjini Kigoma.

Alipoulizwa alikuwa anatarajia nani kuibuka kidedea miongoni mwa makada 41 waliojitokeza kuomba uteuzi wa chama hicho, alisita na kutabasamu kidogo, kisha akasema, “Nilitegemea ningeibuka mimi mshindi.”

Akifafanua zaidi, alisema katika mchuano ule ambao haukuwahi kutokea katika historia ya CCM, kila mgombea alikuwa na matumaini ya kuteuliwa kuwania urais.

Akijibu swali ni mgombea yupi alikuwa tishio kwake kwenye mchuano huo, Birohe kwa sauti ya chini, alisema “Hilo tuliache kama lilivyo.”

Kwa nini tuliache kama lilivyo? Akijibu swali hilo, kada huyo aliyekuwa amevalia sare rasmi ya CCM – suruali nyeusi, shati la kijani na kofia ya kijani, alisema CCM ina utamaduni wake, mgombea akishapitishwa na kuchaguliwa, wengine wote wanakuwa nyuma yake.

 

Mchuano ulivyompaisha

Kada huyo baada ya kupitia katika mchuano huo alitoka akiwa Birohe mwingine kwa kuwa Watanzania wengi walianza kumfahamu tofauti na alivyokuwa awali.

“Watanzania walianza kunifahamu katika habari za siasa, kwamba nilikwenda kugombea urais wa Tanzania,” alisema.

Alisema msukumo wa kuwania urais ulitoka moyoni mwake, tofauti na mawazo ya wengi kwamba huenda alitumwa kufanya hivyo.

“Msukumo huo unatoka moyoni mwangu, hautoki nje. Kila mtu anayo haki na uhuru wa kuchukua fomu kugombea urais, nilianza mchakato wa kuwania urais mwaka 2003 ili nigombee 2005, lakini sababu ambazo hazikuweza kuzuilika wakati ule haikuwezekana, nikajitokeza tena 2015,” alisema.

Alisema mwaka 2003 jina lake halikupewa fursa, lakini safari hii licha ya kukumbana na vikwazo vya wapambe waliokuwa hawataki apewe fomu, alifanikiwa.

“Walikuwapo watu wa pembeni waliokuwa wanataka nisipewe fomu, lakini kwa sababu Chama cha Mapinduzi ni chama pekee chenye mapendo, chenye demokrasia, nikapewa,” alisema.

Alisema baada ya kufanya uamuzi, alimwambia mkewe naye akahoji kwa mshangao.

“Aliniambia, ‘kweli utaweza kufika Dodoma’, nikasema nitaweza. Akasema, ‘utakwenda kuizunguka nchi nzima uiweze’, nikasema nitaweza. Akasema ‘haya, mimi nakutakia safari njema’,” alisema.

 

Gharama za fomu, kusaka wadhamini

Birohe ambaye anajishughulisha na kilimo cha kujikimu alisema hakuna mtu yeyote aliyemchangia fedha Sh1,000,000 za kuchukua fomu na nyingine alizosema nyingi zaidi za kuzunguka kutafuta wadhamini.

“Wakati ule yaliandikwa mengi, madai ya kupewa hela niliyasikia. Wengine walisema sikuwa na pesa nilikuja tu na 600,000, nahitaji kuongezewa 400,000, lakini mimi pesa nilikuwa nazo zote za kuchukulia fomu. Walijaribu kuzungumza mengi sana lakini mimi nilikaa kimya,” alisema.

Alisema maandalizi yake hayakufanyika kwa siku moja, bali yalichukua muda kuanzia mwaka 2000.

Kuhusu fedha za kuzunguka mikoani kutafuta wadhamini alisema alikuwa nazo zote, lakini licha ya kudai kwamba ni nyingi kuliko za kuchukua fomu hakutaka kutaja kiwango chake.

“Zipo za kuzunguka, yaani milioni moja hizo za fomu ni kiasi kidogo sana, hizo za kuzunguka mikoani ni kubwa zaidi, lakini hilo ni fumbo tuliache kama lilivyo... Kweli imeshapita miaka miwili, lakini tuliache, hakuna haja. Hili linabaki kama lilivyo,” alisisitiza Birohe.

Mbali na matumizi ya fedha, katika mzunguko huo wa kusaka fomu, Birohe alisema alikumbana na vikwazo kadhaa, akitolea mfano wa Kisarawe Mkoa wa Pwani, alipokuta wanachama wa kumdhamini wamechukuliwa kwenda kumdhamini mgombea mwingine.

“Nilipofika Kisarawe nilikuta hakuna mtu. Nilimpigia katibu wa wilaya akasema leo hatupo, akasema utusubiri. Niliondoka na kurudi Ilala hadi siku iliyofuata,” alisema.

 

Yaliyotokea Dodoma

Birohe alisimulia kwa nini alionekana kama anatangatanga alipowasili Dodoma kuchukua fomu. Alisema alipofika, moja kwa moja alikwenda benki kuchukua fedha, lakini alipokuwa kwenye foleni alipigiwa simu kwamba zamu yake imefika.

Ndipo akakimbia kwenda CCM makao makuu kuitika wito, kisha akarudi benki kuchukua fedha.

Hata baada ya kupata fedha na kulipia fomu, alisikika akiitikia simu akisema, “tayari mzee”. Alipoulizwa katika mahojiano, huyo mzee alikuwa ni nani, Birohe alisema alikuwa shemeji yake, ambaye hata hivyo, hakutaka kumtaja.

Alipoulizwa kama angefanikiwa Kura za Urais, angefanya jambo gani tofauti na anavyofanya Rais Magufuli, Birohe alisema hilo pia liachwe kama lilivyo na alipoulizwa kuhusu utendaji kazi Rais huyo, alisema kwa ujumla kuwa anafanya vizuri.

Kuhusu jambo gani katika maisha yake akipata fursa atapenda kulirekebisha, alisema ni suala la elimu ili aweze kupata elimu zaidi ya ile ya msingi aliyonayo.

-->