Dawa holela, pombe tatizo kwa watoto

Muktasari:

Baadhi ya wajawazito hunywa dawa bila ushauri wa daktari

Moshi. Unywaji wa pombe kupita kiasi na matumizi ya dawa kwa mjamzito ni chanzo cha ongezeko la kuzaliwa watoto wenye ulemavu na mtindio wa ubongo.

Mkuu wa kituo cha watoto wenye ulemavu cha Shirimatunda, Oliva Mkunde alisema hayo juzi wakati wa ufunguzi wa kisima cha maji kwa ajili ya watoto hao kilichojengwa na shirika lisilo la kiserikali la Umoja Project la Ubelgiji.

“Watoto wenye ulemavu wamekuwa wakiongezeka siku hadi siku kutokana na matumizi ya dawa bila ya kushauriwa na daktari,” alisema Mkunde.

Diwani wa Shirimatunda, Francis Shio alisema Serikali imetakiwa kuwawekea mpango madhubuti watoto wenye ulemavu pindi wanapomaliza elimu ya msingi ili waweze kuanzisha miradi.

Alisema baada ya watoto kumaliza elimu ya msingi wanatakiwa kujitambua kwa kuwa wengi wao wana umri mkubwa.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi, Raymond Mboya aliwataka wakazi wa kata hiyo kutumia vizuri miundombinu na kuitunza ili iwasaidie.

“Tunawashukuru wafadhili wetu kwa kuona umuhimu wa kuwasaidia watoto wetu wenye changamoto,” alisema Meya.

Mwakilishi wa shirika hilo, Henny Schuurmans alisema lengo ni kutoa huduma ya maji kwa kituo cha watoto wenye matatizo ya akili na zahanati iliyopo eneo hilo.

Alisema mradi huo wa maji umegharimu Sh88 milioni.