Thursday, February 16, 2017

Dawa za kulevya zaitikisa dunia

 

By Hussein Issa, Mwananchi hissa@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Karibu katika kila kituo cha mabasi ya daladala kuna vijana ambao baadhi wanazungumza kama wamebana pua, na katika viwanja vya michezo kuna vijana ambao wanavuta sigara zilizotengenezwa kienyeji.

Wale wanaozungumza mithili ya mtu aliyebana pua ni wateja wa mwisho wa dawa za kulevya aina ya heroin na cocaine wakati wale wanaojibanza pembeni mwa viwanja vya michezo ni wavutaji bangi.

Hao ni wateja wanaomudu angalau kiwango kidogo cha cocaine, heroin na bangi ambacho bei yake ni rahisi kwa kuangalia uwezo wao wa kiuchumi. Ukiangalia jinsi sehemu hizo zilivyo nyingi na zinazohusisha watu wengi, unapata picha ya kiwango cha matumizi ya dawa za kulevya nchini.

Wako ambao wameamua kuachana na matumizi ya vilevi hivyo na sasa wanapata matibabu katika kliniki maalumu na wako ambao wameshaharibikiwa akili kutokana na kutumia dawa hizo kupita kiasi.

Na wako ambao wameshapoteza maisha ama kwa kujidunga dawa hizo kupita kiasi, au kupata magonjwa yanayohusiana na dawa hizo zilizoharamishwa.

Ni dhahiri kuwa mazingira hayo yanahalalisha vita yoyote dhidi ya dawa za kulevya duniani, vita inayohitaji nguvu za ziada kutokana na ujanja wa wauzaji na nguvu kubwa waliyonayo kifedha.

Wiki iliyopita, Serikali iliongeza nguvu katika vita hiyo kwa kuteua viongozi wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, ikiwa ni kutimiza mahitaji ya sheria mpya, baada ya Rais John Magufuli kumteua Rogers Sianga kuwa kamishna mkuu wa chombo hicho.

Kabla ya kuteua watu hao, tayari wanasiasa, viongozi wa dini, wafanyabiashara wakubwa na wasanii wa filamu na muziki walishaitwa polisi kuhojiwa kuhusu matumizi na biashara ya dawa hizo na baadhi yao kupelekwa mahakamani na wengine kushikiliwa kwa siku kadhaa.

Kwa mujibu wa ripoti ya Dawa za Kulevya ya Mwaka 2016 iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa (UNODP), mtu mmoja kati ya 20 walio na umri kati ya miaka 15 na 64 alitumia angalau dawa aina moja ya kulevya kwa mwaka 2014.

“Hata hivyo, wakati zaidi ya watu milioni 29 waliotumia dawa za kulevya wanakisiwa kuwa na matatizo ya kiafya yatokanayo na matumizi hayo, na kati yao milioni 12 ambao walitumia sindano kujidunga na ambao asilimia 14 kati yao wanaishi na Virusi vya Ukimwi, athari za matumizi ya dawa za kulevya kwa kuangalia madhara ya kiafya, zinaendelea kuwa kubwa,” inasema ripoti hiyo ya UNODP.

“Huku kukiwa na vifo vinavyokisiwa kufikia 207,400 vinavyotokana na dawa za kulevya kwa mwaka 2014, idadi ambayo ni sawa na asilimia 43.5 ya vifo vya mamilioni ya watu walio na umri kati ya miaka 15-64, idadi ya vifo vinavyohusishwa na dawa hizo duniani haijabadilika, licha ya kwamba suala hilo halikubaliki na linazuilika.”

Amerika Kaskazini inaongoza kwa vifo vinavyotokana na dawa za kulevya ikiwemo kuongezeka kwa vifo vya kuzidisha dozi  na kuongezeka kwa madhara ya kiafya na kiusalama kwa raia yatokanayo na matumizi ya bangi kwenye nchi za Marekani na Canada.

Mwenyekiti chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira amesema suala la dawa za kulevya ni vita ya kimataifa, wala si ya kitaifa ndio maana wanaohusika wanakuwa na majina makubwa.

Alisema ni vyema wananchi wakatoa ushirikiano kuhakikisha tatizo hili linafikia kikomo kwa kuwataja wahusika wa dawa hizo na wala si kuwataja wale wadogo.

“Hii ni vita ambayo jamii haitakiwi kurudi nyuma kuhakikisha tunashinda mapambano haya kwa nguvu zote ili tuokea vizazi vyetu,’’ alisema Mghwira ambaye aligombea urais katika uchaguzi uliopita.

Kalama Masoud ‘Kalapina’, ambaye ni mwanaharakati, alisema suala la dawa za kulevya linachukuliwa kisiasa zaidi badala ya kupambana nalo.Alisema mtu akibainika kwamba anajihusisha na dawa za kulevya, anatakiwa kupatiwa matibabu mara moja na si kuachiwa azungumze kwenye hadhara wakati bado ni muathirika.

“Nimeshangaa msanii ameshabainika kwamba anatumia dawa za kulevya, lakini kesho yake anashika kipaza sauti na kusema anaomba radhi. Huyu bado ni mwathirika wa dawa na anatakiwa apatiwe matibabu kwanza,” alisema.

Naye mtayarishaji wa muziki nchini, Sweatbert Charles alisema wasanii wengi wanaotumia dawa za kulevya wanatumika kuzisafirisha kutokana na ulimbukeni wao huku wakijua zina madhara kwa afya yao.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya UNODC, biashara hiyo ndiyo uhalifu mkubwa duniani na inachukua asilimia 50 ya uhalifu wa kupanga.

Dawa zilizo katika biashara hiyo haramu ni methamphetamine, cocaine, ambayo inajulikana zaidi kama unga, bangi, heroin na oxycodone. Kibaya zaidi, ripoti ya UNODC inaonyesha mzunguko wa kifedha wa biashara ya dawa za kulevya duniani una thamani ya dola 435 bilioni za Kimarekani (sawa na Sh972 trilioni za Kitanzania).

Ripoti nyingine ya Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za kulevya (INCB) kuhusu Afrika na Tanzania ya mwaka 2015, inaonyesha usafirishaji wa heroin kupitia nchi za Afrika Mashariki umeongeza matumizi ya dawa hizo zinazotoka Afghanistan.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, eneo la Amerika ya Kati limeendelea kuwa msambazaji mkubwa wa bangi na njia ya kupitishia cocaine kwenda nchi za Amerika Kaskazini na Ulaya.

Ripoti ya mwaka 2013 ya UNODP inaeleza sababu kubwa za kuzigeuza nchi za Afrika Mashariki kuwa kituo kikubwa cha kupitishia dawa hizo ni pamoja na mipaka kutokuwa na ulinzi mkali.

“Afrika Mashariki ni eneo ambalo wasafirishaji dawa wanalenga kulitumia kuingia katika soko la Afrika kwa sababu ya pwani zake kutokuwa na udhibiti, kuwa na bandari kubwa na viwanja vya ndege na mipaka yenye mianya mingi, ambayo inatoa nafasi ya sehemu nyingi za kuingilia na kutokea,” inasema ripoti hiyo.

Tovuti ya UNODP inaeleza kuwa katika kipindi cha mwaka 1995-2006, kuliripotiwa matukio ya kukamatwa kwa heroin, bangi na cocaine eneo la Afrika Mashariki ambayo ni machache na hayaonyeshi kiwango kikubwa cha usafirishwaji, uwepo na ongezeko la matumizi ya dawa hizo.

“Kwa hiyo, idadi ndogo ya matukio ya kukamatwa kwa dawa hizo ni ishara kwamba udhibiti mipakani ni dhaifu kuliko ishara kwamba hakuna dawa zinazosafirishwa kupitia kanda hiyo,” inaeleza tovuti hiyo.

“Mapitio ya kuanzia mwaka 1998 hadi sasa yanaonyesha kuwa kuna ongezeko kubwa la usafirishaji wa dawa aina ya heroin kuingia Afrika Mashariki zikitokea Pakistan, Thailand na India. Ongezeko la kukamatwa kwa heroin inayo na uhusiano na Nigeria ambazo zilikuwa zikipelekwa Uganda, Tanzania na Kenya kupitia Ethiopia yamerekodiwa.

“Takwimu na ukamataji zinaonyesha kuwa idadi ya Watanzania na raia wa Msumbiji wanaoshiriki katika usafirishaji heroin kutoka Pakistan na Iran inazidi kukua.”

Kilimo cha cocaine kimeongezeka kwa asilimia 44 mwaka 2014  nchini Colombia tofauti na miaka ya nyuma wakati kimeendelea kupungua kwenye nchi za Bolivia na Peru.

Dawa jamii ya amfetamini hasa metamfetamini zimeendelea kuwa tishio kwenye eneo la Asia ya Mashariki na Kusini-Mashariki mwa Asia. Kujitokeza kwa dawa mpya za kulevya kumeongeza wasiwasi.

Kwenye eneo la Asia Kusini kumekuwa na ongezeko la utengenezaji, usafirishaji na matumizi ya metamfetamini. Halikadhalika, uchepushaji na matumizi ya dawa za tiba zenye madhara ya kulevya umeendelea kuwa changamoto kubwa.

Kupungua kwa usalama na kuongezeka kwa migogoro kwenye baadhi ya nchi za Asia Magharibi kumesababisha wakimbizi ndani na nje ya eneo hilo na kuongeza uwezekano wa magenge ya kihalifu kufanya biashara ya dawa za kulevya na hatimaye kuongezeka kwa matumizi.

Idadi ya dawa mpya za kulevya zilizogunduliwa mwaka 2014 Ulaya Magharibi na Kati imeendelea kuongezeka kwenye nchi za Ulaya Mashariki na Kusini-Mashariki mwa bara hilo, viwango vya matumizi na kujidunga dawa za kulevya ni takribani mara tano zaidi ya wastani duniani. Kwa mujiblu wa ripoti hiyo bara la Afrika liliendelea kutumika kupitisha dawa za kulevya. Afrika Magharibi inatumika mara kwa mara kupitisha cocaine na dawa nyingine kuelekea bara la Ulaya wakati Afrika ya Kaskazini iliendelea kuwa chanzo kikuu cha dawa zilizoingia barani Ulaya.

Kutumika kwa Afrika ya Mashariki kama kitovu cha kusafirisha heroin iliyotokea Afghanistan ikipelekwa bara la Ulaya, kuliongezeka. Hali hii inachukuliwa kuwa ndiyo sababu ya kuongezeka kwa matumizi ya heroin katika eneo la Afrika ya Mashariki.

Wafanyabiashara wa dawa za kulevya waliwalenga watu wenye kipato cha kati ili kuongeza masoko ya dawa hizo katika nchi ambazo biashara hiyo ilipitia zikiwemo za Benini na Namibia.

Ongezeko la biashara ya dawa za kulevya barani Afrika, limeongeza idadi ya watumiaji wa dawa za kulevya hasa vijana wadogo na kuongeza  vitendo viovu vinavyofanywa na magenge ya kihalifu.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa eneo la Afrika ya Magharibi na Afrika ya Kati, uhalifu wa kimtandao ulisababisha madhara makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa kukuza biashara ya dawa za kulevya na kuongeza idadi ya wagonjwa wa dawa za kulevya pamoja na kusababisha wahalifu wachache wenye silaha kuhodhi madaraka na mali nyingi.Ingawa kumekuwepo na jitihada zinazofanywa na nchi za Magharibi mwa Afrika kupitia Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (Economic Community of West Africa-Ecowas), kwa ujumla  biashara ya dawa za kulevya na matumizi ya dawa hizi katika eneo hili yameongezeka.

Kwa mujibu wa mamlaka zinazosimamia sheria nchini Afrika Kusini, makundi ya kusafirisha dawa za kulevya kutoka China na eneo la

Jumla ya kilo 387 za heroin (zilikamtwa kwa mkupuo mmoja katika bandari ya Mombasa), lita 3,200 za maji yaliyochanganywa na heroin na lita 2,400 za mafuta ya dizeli yaliyochanganywa na heroin zilikamwatwa nchini Kenya mwaka 2014.

Jumla ya kilo 321 za heroin zilikamatwa Tanzania mwaka 2014.

Hivi sasa, ripoti mbalimbali zinaonyesha wasafirishaji wa dawa hizo sasa wanatumia usafiri wa meli kubwa ambazo hutia nanga katika bahari kuu na kushusha mizigo yenye dawa hizi kwenye majahazi, mashua, boti ziendazo kasi au hata ngalawa ambazo husafirisha mizigo hiyo hadi nchi kavu.

Ann Fordham wa Taasisi ya Kimataifa ya Sera za Dawa za Kulevya, anasema vita ya dawa za kulevya ikabiliwa na tatizo kubwa la kisera.

Biashara hiyo inakabiliwa na kikwazo kingine ambacho ni baadhi ya serikali, hasa za Amerika Kusini kufanya dawa hizo zisiwe haramu.

-->