Deni la Sh600,000 lazuia maiti ya kichanga kutolewa Muhimbili

Mkazi wa Ukonga Mombasa kwa Diwani Jijini Dar es salaam,Hamida Gwota aliyezuiwa mwili wa mwanae mchanga usichukuliwe katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa deni la sh631,584 za matibabu .Picha na Tumaini Msowoya

Muktasari:

  • Hamida alitakiwa kulipa fedha hizo baada ya mwanaye wa siku nne aliyezaliwa utumbo ukiwa nje, kufariki dunia wakati akitibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Mei 12.

Dar es Salaam. Pamoja na uchungu wa kuzaa, uchungu wa kifo cha mtoto wake mchanga lakini Hamida Gwota alizuiwa kuondoka hospitali kwenda kumzika mwanaye hadi alipe deni la Sh631, 584 za matibabu ya mtoto aliyefariki dunia.

Hamida alitakiwa kulipa fedha hizo baada ya mwanaye wa siku nne aliyezaliwa utumbo ukiwa nje, kufariki dunia wakati akitibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Mei 12.

Kwa mujibu wa Sera ya Afya, matibabu ya mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano ni bure. Lakini Hamida hakupata huduma hiyo.

“Nilizuiwa kuchukua mwili wa mwanangu mpaka ndugu walipofanikiwa kukusanya Sh631,584 ili kulipia gharama za matibabu,” alisema Hamida katika mazungumzo na Mwananchi nyumbani kwake Ukonga jijini Dar es Salaam, juzi.

“Mwanangu alifariki Mei 12, lakini nilizuiwa kutoka. Ilibidi nilale wodini huku mwili wake ukiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti hadi fedha zilipopatikana ndipo nikakabidhiwa.”

Hamis Gwota, baba mzazi wa Hamida, alisema alipopata taarifa ya kifo cha mjukuu wake alienda kuomba aelekezwe hatua anazopaswa kufuata ili wakabidhiwe mwili.

“Nilipouliza nikaambiwa kuna bili na lazima ilipwe ndipo watupatie. Binafsi nilishangaa kwa sababu siku zote nimekuwa namsikia waziri wa Afya anasema mtoto chini ya miaka mitano hutibiwa bure,” alisema Gwota.

Alisema ilibidi waitishe kikao cha ndugu ili kuchangishana hadi zilipopatikana fedha hizo.

“Kwa hiyo wakati tunachangishana fedha, mwanangu aliendelea kubaki wodini hadi siku ya pili tulipokabidhiwa mwili baada ya kukamilisha malipo yote.

“Nilijisikia vibaya lakini sikuwa na namna nyingine zaidi ya kuhangaikia fedha hizo.”

Gwota alisema kama ndugu wasingechangishana, basi binti yake angeendelea kusota wodini.

Naye Hamida alisema awali alitegemea bima yake ya afya ya NHIF ingemwezesha kugharimia matibabu ya mwanaye aliyezaliwa akiwa anaumwa, lakini haikuwa hivyo.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma cha MNH, Aminiel Aligaesha alisema kwa mujibu wa sera za hospitali hiyo mgonjwa yeyote aliyepewa rufaa akitokea hospitali binafsi, hupokewa na kutibiwa kama mgonjwa binafsi.

“Hii haijalishi ni mama mjamzito au mtoto. Hiyo ndiyo sera yetu na ipo wazi kabisa katika hilo eneo,” alisema.

Kujifungua kwa njia ya upasuaji

Hamida alisema awali baada ya kupata uchungu aliamua kwenda kujifungua katika Hospitali ya Kairuki jijini Dar es Salaam, kwa sababu alikuwa na bima ya afya.

“Nilijifungua kwa njia ya upasuaji Mei 7, bahati mbaya mwanangu alizaliwa na tatizo la utumbo kuwa nje hivyo tulipewa rufaa hadi Muhimbili,” alisema.

Alisema lengo la kupelekwa MNH lilikuwa kuurudisha utumbo ndani.

Mama huyo alisema kabla ya mtoto wake kupewa kitanda wodini, aliambiwa wazi kwamba kwa sababu alipata matibabu ya awali hospitali binafsi, ilibidi ajigharimie.

Alisema baada ya kupewa maelezo hayo alilazwa na mwanaye.

“Kwa hiyo niliambiwa kila baada ya saa tatu niende kumuona mwanangu, nikawa nafanya hivyo,” alisema Hamida.

Alisema siku moja kabla ya kifo, mtoto alianza kubadilika, jambo lililomkatisha tamaa.

Alisema aliendelea kwenda kumuona mwanaye kama alivyoelekezwa, japo alilazimika kukabiliana na hali ya kupanda na kushuka ngazi hadi ghorofa tatu.

“Hata hivyo sikuchoka kwenda kumtazama mwanangu. Kutokana na hali yake hakuwa akinyonya kabisa,” alisema.

Alisema siku aliyofariki dunia, alienda kumuona kama kawaida lakini alipofika chumba alicholazwa, aliona hali tofauti.

“Nilifika pale nikakuta mwanangu ametoa macho na nilipomchunguza, nikagundua amefariki. Ikabidi nianze kupiga kelele kumuita nesi ili walau anisaidie kumtengeneza,” alisema.

Lakini Hamida bado anasikitishwa na kitendo cha kumtaka agharimie matibabu ya mwanaye.

“Kama kujifungulia hospitali binafsi ni kosa linaloweza kusababisha mtoto chini ya umri wa miaka mitano asipewe msamaha wa matibabu, Serikali ingepaswa kutangaza wajawazito wote kujifungua hospitali zake,” alisema.

“Hivi ni dhambi kujifungulia hospitali binafsi ambayo pia sikutumia pesa zangu isipokuwa bima? Ni kwa nini mwanangu abaguliwe kwenye sera? Najiuliza maswali mengi bila majibu lakini ilibidi niuvumilie usiku wote niliofiwa hadi pale nilipopewa mwanangu akazikwe.”

Mkurugenzi wa tiba na ushauri wa kiufundi wa NHIF, Dk Aifena Mramba alisema bima ya afya ya mtoto hupatikana kulingana na idadi ya wategemezi wa mzazi wake.

“Kwa hiyo kama idadi ya wategemezi inaruhusu, bima ya afya ya mtoto inatolewa ndani ya siku moja. Kwa hiyo (wafanyakazi wa) mapokezi kwenye hospitali husika wangeweza kuwasiliana nasi kwa kile kinachoendelea,” alisema.

Hata hivyo alisema ili kuokoa maisha ya mgonjwa, matibabu yanaweza kuendelea katika hospitali iliyo na mgonjwa wakati bima hiyo ikiendelea kuandaliwa na huwa inakamilika ndani ya siku moja.

Baba wa mtoto huyo, Hafidhu Mustapha alisema alichoambulia ni kuona kaburi la mwanaye kwa kuwa kipindi chote cha kuzaliwa, kuugua hadi kufariki dunia alikuwa safari.