Wednesday, June 13, 2018

Dismas Komba, fundi simu anayefanyia kazi kitandani

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi

Hujafa, hujaumbika, hayo ndio maneno unayoweza kuyatumia kwa Dismas Komba, mkazi wa Minarani wilayani Ifakara, mkoani Morogoro.

Komba ambaye alizaliwa miaka 38 iliyopita, wilayani Malinyi na kusoma Shule ya Msingi Mtimbila, alijikuta akipata ulemavu baada ya kuangukiwa na kifusi cha mchanga.

Katika mahojiano yake na Mwananchi, Komba anasema kwamba baada ya kumaliza elimu ya msingi hakufanikiwa kuendelea na kidato cha kwanza, matokeo yake hayakuwa mazuri.

Baada ya kuwa na matokeo mabaya, mama yake akamshauri kutafuta chuo cha ufundi, ambapo alienda kusomea Chuo cha Ufundi Chala, Sumbawanga, ambapo alisoma huko kozi ya ufundi selemara mwaka 1997.

Baada ya hapo ndio akaenda wilayani Ifakara kwa ajili ya kujitafutia kazi ili iwe kama mtaji wa kumuwezesha kukusanya vifaa vya kufungua ofisi yake.

Katika harakati za kutafuta kazi, Komba anasema kwamba aliishia kupata kibarua cha kuchimba mchanga katika machimbo ya Shungu.

Inaendelea UK 26

Inatoka UK 25

Akiwa katika kazi hiyo anasema anakumbuka ilikuwa Septemba 24, 2013, akiwa amejipumzisha katika moja eneo ambapo shughuli za uchimbaji mchanga zinafanyika, kifusi kilimdondokea na kumfunika kabisa kama mtu aliyezikwa.

“Hata hivyo katika watu kupambana kuniokoa walifanikiwa lakini kwa bahati mbaya nilipofikishwa hospitali niligundulika kuwa nimepata tatizo katika uti wa mgongo jambo lililonifanya nishindwe kukaa.

“Kuanzia hapo ndio nikawa mlemavu wa kudumu hadi hii leo unaponiona nimelala hapa kitandani, japokuwa huko nyuma nilitumia baiskeli kwenda kutafuta riziki, lakini tangu nitokewe na kidonda pajani miezi sita iliyopita nilijikuta nashindwa kufanya hivyo kuishia kufanya kila kitu nikiwa nimelala.

Mbali na hilo Komba pia anasema kutokana na ulemavu huo hata mke aliyekuwa akiishi naye na kuzaa naye watoto wawili amemkimbia na sasa anahangaika mwenyewe katika kuwalea watoto hao.

Anavyozikabili changamoto za maisha

Pamoja na hali aliyonayo, Komba anasema anamshukuru Mungu alikuwa mmoja wa walemavu sita waliopewa mafunzo ya ufundi wa kutengeneza simu kupitia mradi wa kuwezesha vijana kiuchumi wa YEE unaosimamiwa na Shirika la Plan International.

Shirika hilo mbali na kutoa mafunzo kwa vijana, pia wanapohitimu huwapa vifaa vya kuanzia kazi, huku Komba akiwa mmoja wa wanufaika hao.

Katika ufundishaji huo, Komba anasema kwamba kutokana na hali yake, mwalimu alikuwa akienda nyumbani kwake kumfundisha, kazi ambayo ilifanywa na mwalimu huyo kwa wastani wa miezi 10.

“Baada ya kumaliza mafunzo yangu, nashukuru walinipatia baadhi ya vifaa ambavyo kutokana na kazi zetu hizi kuhusisha umeme baadhi ya vifaa hivyo vimeshaungua na sasa naazima kwa watu pindi ninapopata mteja.

“Pia kutokana na kuwa ni mtu wa kulala ndani, hata wateja kuwapata inakuwa tabu, wanakuja mmoja mmoja tofauti na ambavyo ningekuwa na ofisi eneo ambalo limechangamka,” anasema.

Kutokana na hali hiyo, Komba anawaomba wadau mbalimbali kujitokeza kumsaidia ikiwemo kupata matibabu ya kidonda kinachomsumbua ili anyanyuke tena.

Pia anawaomba kumpatia vifaa ambavyo ataweza kufanyia kazi zake na eneo la kufanyia kazi ambalo itakuwa rahisi wateja kumuona tofauti na ilivyo sasa mpaka wafike nyumbani.

Alivyoingizwa katika mradi wa Plan

Raymond Kanyambo, Mratibu wa Mawasiliano wa Plan International, anasema mradi wa YEE ulioanza mwaka 2016, unalenga kufikia jumla ya vijana 9,100, huku asilimia 10 wakiwa walemavu.

Kwa hiyo Komba akawa mmoja wa walemavu wa viungo watano katika wilaya ya Ifakara waliopewa elimu ya ujuzi wa kutengeneza simu na ujasiriamali kupitia mradi huo.

Kanyambo anasema pamoja na kuhitimu na kuwapa vifaa vya kuanzia kazi, moja ya changamoto inayowakabili katika kujikomboa kiuchumi ni pamoja na kupata wateja, mitaji ya kuendeleza kazi zao na vifaa vya kutosheleza.

Mtoto wake anasemaje

Mtoto wa kwanza wa Komba, Desderia Komba (12), anasema anasikitika tangu baba yake apate ajali wamekuwa wakiishi maisha ya tabu ukizingatia na mama yao ameondoka.

Anasema wakati mwingi wanapokwenda shule inabidi wamuandalie vitu vya kupika baba yao karibu na kitanda anacholala ili awapikie chakula cha jioni.

“Unajua wakati mwingine mimi na mdogo wangu Desderius (8), tunachelewa kurudi shule hivyo baba anaona katika muda ambao anakuwa amelala bora anisaidie kupika ili nami ninaporudi niendelee na shughuli nyingine kama za kuosha vyombo na usafi mwingine,”anasema.

Hata hivyo anakiri imekuwa kazi ngumu kwake kwani kuna wakati anakosa hata muda wa kusoma kutokana na kuchoka na kazi japo anaeleza kwamba kamwe hawezi kukaa mbali na baba yake pamoja na matatizo anayoyapitia.

Anaongeza kwamba hata kula wakati mwingine wanasubiri hadi apite msamaria mwema wa kumsaidia baba yao ndio wabandike sufuria jikoni.

Ombi lake kwa wadau, kuwasaidia kuwapa madaftari na hata nyumba kwani nyumba wanayokaa ni ya chumba kimoja walichopewa na babu yake mdogo na kila kitu wanafanyia huko ndani huku yeye akiwa anaombewa kulala kwa majirani.

Mama mkwe afunguka

Mama mkwe wa Komba, Asia Mohamed anasema kitendo kilichofanywa na mtoto wao kumkimbia mwenzake akiwa katika matatizo hakijawafurahisha hata wao.

Asia anasema wamefanya kila njia yeye na mumewe kumshawishi mtoto wao huyo amrudie mwenzake lakini imeshindikana na tayari ameolewa na mwanaume mwingine. “Kama wazazi tumefanya kila jitihada kumrudisha mtoto wetu ili aje alee familia na mumewe lakini imeshindikana, kwa hiyo msaada wetu tunaofanya ni kile kidogo tunachokipata tunagawana ili naye asione kama ametengwa.

Majirani wazungumza

Mmoja wa majirani zake aliyejitambulisha kwa jina la Fatuma Mkulila, anasema kutokana na maisha yao kuwa ya kawaida, huwa wanamsaidia Komba pale anapokwama kama vile amepungukiwa mchele, unga au mboga.

Fatuma anasema wadau wana kila sababu ya kujitokeza kumsaidia kaka huyo, ambaye anasema kila wakimuangalia mazingira anayoishi hawaoni kama ana raha ya dunia na hasa watoto wake ambao wanamtegemea kwa kila kitu.

Pia anasema mazingira anayoishi hastahili kuishi binadamu wa sasa, hivyo kama kuna mdau atajitokeza atakuwa kamsaidia kwa kiasi kikubwa.

Msaada kwa familia

Mama mdogo wa Komba, Asteria Lipandika, anasema walimlea Komba tangu mdogo hadi kufikia hatua ya kujitegemea lakini alipata tatizo akiwa katika maisha yake ya kujitafutia, na wao kama familia wasingeweza kumtupa, ingawa kwa sasa inakuwa ngumu kukidhi mahitaji yake yote kwa kuwa tayari naye ana familia ya watoto wawili.

“Kama unavyoona na sisi umri wetu umeenda, hatuwezi kukidhi mahitaji yote ya Komba pamoja na yale ya watoto wake, ndio maana tunaomba na wadau wengine wajitokeze kumsaidia.’’

-->