Ditto, Gabo wanyakua tuzo ZIFF

Muktasari:

Wakati Ditto akijinyakulia tuzo ya video bora, Gabo ameshinda tuzo ya muigizaji bora

Zanzibar. Msanii wa Bongo Fleva, Lameck Ditto na muigizaji wa Bongo Movie, Salim Ahmed maarufu Gabo wamejinyakulia tuzo katika tamasha la filamu Zanzibar (Ziff) zilizotolewa usiku wa kuamkia leo Jumapili Julai 15, 2018.

Wakati Ditto akijinyakulia tuzo ya video bora, Gabo ameshinda tuzo ya muigizaji bora.

Ditto ameshinda tuzo hiyo kupitia video ya wimbo wake wa Nabembea. Mwaka 2017 tuzo hiyo ilichukuliwa na msanii FQ kupitia video ya wimbo wake wa Walk it off.

Kwa upande wa Gabo ameshinda tuzo ya muigizaji bora wa kiume kupitia filamu ya In Segere.

Tuzo hiyo ni ya pili kunyakuliwa na muigizaji huyo katika tamasha hilo, mwaka 2017 alichukua tuzo kupitia filamu yake ya Safari ya Gwalu.

Hata hivyo, wasanii hao hawakuwepo na badala yake tuzo hizo zilichukuliwa na wawakilishi wao.

Tamasha hilo la Ziff linafanyika katika viwanja vya Ngome Kongwe visiwani hapa.