Diwani wa tisa Chadema ajiuzulu mkoani Arusha

Diwani wa Kata ya Moita (Chadema), Edward Sapunyo (kulia) akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Monduli, Steven Ulaya barua yake ya kujiuzuru udiwani, mkoani Arusha juzi. Na Mpigapicha Wetu

Muktasari:

Mkurugenzi huyo akizungumza na mwandishi wa gazeti hili alithibitisha kupokea barua hiyo.

Arusha. Madiwani wa Chadema wameendelea kukihama chama hicho kwa kile wanachodai ni katika kuunga mkono utendaji kazi wa Rais John Magufuli.

Diwani wa Moita katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Edward Sapunyo alijiuzulu wadhifa huo na kufikisha idadi ya madiwani tisa waliofanya hivyo.

Jana alikabidhi barua ya kujiuzulu kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Steven Ulaya.

Mkurugenzi huyo akizungumza na mwandishi wa gazeti hili alithibitisha kupokea barua hiyo.

Ulaya alisema akiwa msimamizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo atapeleka taarifa ngazi za juu kwa ajili ya utaratibu wa uchaguzi mdogo.

“Moja ya jambo lililoniuma kuna mradi wa maji ambao nimehangaika nao tangu mwaka 2006 fedha zilipatikana na umekuwa unaendelea vizuri, lakini viongozi wangu wanaukwamisha usifikie tamati licha ya kuwa wananchi wameanza kutumia maji,” alisema Sapunyo, ambaye amewahi kuwa mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Monduli 2011 hadi 2015.

Katibu wa CCM Wilaya ya Monduli, Gurisha Mfanga amemkaribisha diwani huyo katika chama hicho.