Dk Mary Nagu ashikiliwa kwa muda polisi

Muktasari:

Dk Nagu alifikishwa kituoni kutokana na vurugu zilizoibuka kwenye kikao cha kamati ya siasa ya CCM Wilaya ya Hanang.

Arusha. Mbunge wa Hanang (CCM), Dk Mary Nagu ameshikiliwa kwa muda polisi baada ya kutokea vurugu katika kikao cha kamati ya siasa ya chama hicho.

Dk Nagu aliyewahi kuwa waziri katika wizara kadhaa wakati wa utawala wa Serikali za awamu mbili zilizopita, alishikiliwa kwa muda leo, Julai 18 na kuachiwa baada ya kuhojiwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Francis Masawe amesema Dk Nagu alifikishwa kituoni kutokana na vurugu zilizoibuka kwenye kikao cha kamati ya siasa ya CCM Wilaya ya Hanang baada ya makundi mawili kujitokeza.

Masawe amesema baada ya mahojiano kufanyika na kuandika maelezo, kwa kuwa mgogoro huo ulikuwa ni mambo ya ndani ya CCM walimwachia.

"Taarifa ambazo nimepata ameachiwa baada ya kuandika maelezo na tayari walifikia makubaliano wenyewe," amesema.

Awali, mkuu wa wilaya hiyo, ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya siasa ya wilaya, Sara Msafiri amesema: "Ni kweli amekamatwa lakini nipo kwenye kikao siwezi kuzungumza.”

Habari kutoka ndani ya kikao hicho, zimeeleza Dk Nagu alikamatwa kutokana na malumbano ya kupitisha wagombea wa uchaguzi ndani ya CCM.