Dk Mndolwa azungumzia uongozi wake

Muktasari:

Haidary Haji Abdallah amechaguliwa kuwa makamu mwenyekiti kwa kura 462.

Dodoma. Wajumbe wa mkutano mkuu wa tisa wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, wamemchagua Dk Edmund Mndolwa kuwa mwenyekiti wa Taifa wa jumuiya hiyo kwa kura 552 kati ya kura 811 zilizopigwa.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM aliyesimamia uchaguzi huo, Jerry Silaa alimtanga mshindi Dk Mndolwa jana Jumanne Desemba 12,2017.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Dk Mndolwa amesema atakuwa mkali katika mambo ya utawala bora na atakomesha vitendo vya rushwa.

“Nimeomba uongozi kwa sababu nataka kukitumikia chama, nataka nitumikie kwa moyo wangu wote, kwa akili yangu yote na kwa uwezo wangu wote,” amesema.

Amesema kipaumbele chake ni kufanikisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka 2019.

Amesema atahakikisha jumuiya hiyo inajitegemea kwa sababu yeye ni mchumi; kuboresha masilahi ya wafanyakazi wa jumuiya hiyo; na kumaliza madeni ya ndani ya watumishi.

 

Mbali na Dk Mndolwa, wajumbe wa mkutano huo wamemchagua Haidary Haji Abdallah kuwa makamu mwenyekiti kwa kura 462 akimshinda Mwantumu Mussa Sultan aliyepata kura 282.

 

Msimamizi wa uchaguzi huo Silaa, amesema uchaguzi wa nafasi ya makamu mwenyekiti ulirudiwa baada ya wagombea wanne waliowania nafasi hiyo kushindwa

kupata nusu ya kura zilizopigwa.

Wajumbe wamewachagua Namelock Sokoine, Paul Kirigini, Salum Kinginte, Suleiman Kimea na Amina Ali Mohamed kuwakilisha jumuiya hiyo katika Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.

Makamu Mwenyekiti wa CCM -Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema jumuiya hiyo katika miaka ya karibuni ilipata changamoto nyingi.

Amesema kuna wakati ilikuwa taabani lakini mwenyekiti aliyemaliza muda wake Abdallah Bulembo alifanya kazi ya kutatua changamoto hizo.

Amesema jumuiya hiyo ina kazi kubwa katika kipindi cha miaka mitano lakini anaamini wanachama watashirikiana na viongozi ili iende kwa kasi.

Dk Shein amewataka wanachama ambao kura zao hazikutosha wasikate tamaa kwa kuwa uchaguzi ni utaratibu wa kidemokrasia.