Waziri wa Fedha atoa takwimu ukuaji uchumi

Muktasari:

Dk Mpango afananisha ukuaji uchumi na mwendo wa gari.

Dar es Salaam. Serikali imesema katika nusu ya kwanza ya mwaka 2017, kuanzia Januari hadi Juni, pato la Taifa limekua kwa asilimia 6.8 ikilinganishwa na asilimia 7.7 ya kipindi kama hicho mwaka jana.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema hayo leo Desemba 29,2017 alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa uchumi wa Taifa, utekelezaji wa bajeti mwaka 2017/18,  changamoto na matarajio ya Serikali mpaka Juni. 

Amesema tofauti ya mwaka 2016 na huu wa 2017 haina maana kuwa uchumi umeporomoka.

"Ukuaji wa uchumi ni kama mwendo wa gari. Unaweza kwenda Morogoro kwa kasi au taratibu na wote mtafika. Barabarani kuna mambo mengi yanayofanya usiende kasi. Hata kasi ya ukuaji uchumi ni vivyo hivyo," amesema.

Akizungumzia kasi ya ukuaji uchumi ya kitakwimu kutoendana na maisha ya wananchi amesema, "Ili kasi ya uchumi iweze kunufaisha wengi ni lazima watu wafanye kazi katika sekta zinazokua haraka."

"Hapa nchini wengi wapo katika kilimo ambacho kinakua kwa kasi ndogo," amesema.

Akieleza jinsi uchumi wa Tanzania ulivyo tofauti na nchi nyingine za Afrika Mashariki,  amesema mwaka huu utakua kwa asilimia saba.