Dk Nchemba awajibu wanaosema bajeti ya Serikali ni hewa

Muktasari:

Dk Nchemba amesema ni lazima kufunga mkanda na kujenga misingi itakayoiwezesha nchi kujitegemea.

Moshi. Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba, amesema wanaosema bajeti ya mwaka huu ni hewa, hawaelewi maana halisi ya bajeti.

Dk Nchemba amesema hayo leo Juni 17, 2018 wakati wa mahafali ya kwanza ya vijana wa CCM wa vyuo vikuu vya Mkoa wa Kilimanjaro.

Amesema kuna watu wameibuka wakidai bajeti ya Serikali ya mwaka 2018/19 ya Sh32.47 trilioni iliyowasilishwa Juni 14 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ni hewa jambo ambalo si sahihi.

Dk Nchemba amesema haijawahi kutokea bajeti ya maendeleo kuwa hewa, hivyo wanaozungumza na kujadili kwenye mitandao ya kijamii kuwa ni hewa hawaelewi maana halisi ya bajeti.

"Unapanga makadirio ya matumizi kwa makusanyo na siku zote bajeti ambayo inafanya mambo yanayoonekana haiwezi kuwa hewa. Mambo anayoyafanya Rais kwa sasa ni kujenga misingi na wanufaika ni sisi vijana na watoto wetu," amesema.

Dk Nchemba amesema ni lazima kufunga mkanda na kujenga misingi itakayoiwezesha nchi kusimama na kujitegemea.