Dk Shein afanya mabadiliko Baraza la Mawaziri Zanzibar

Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein


Muktasari:

  • Katika mabadiliko hayo, shughuli za vijana zimehamishiwa katika Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo, shughuli za mazingira zimehamishiwa katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na shughuli za Wakala wa Serikali wa Uchapaji zimehamishiwa wizara mpya ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale.

Zanzibar. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein amefanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri kwa kuongeza wizara moja, kuwabadilisha wizara baadhi ya mawaziri.

Katika mabadiliko hayo, shughuli za vijana zimehamishiwa katika Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo, shughuli za mazingira zimehamishiwa katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na shughuli za Wakala wa Serikali wa Uchapaji zimehamishiwa wizara mpya ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale.

Katika mabadiliko hayo, pia amewateua manaibu waziri wapya wawili na kumbadilisha wizara naibu waziri mmoja na kuifanya Serikali ya Zanzibar kuwa na wizara 14.

Baraza la Mapinduzi

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Ussi Gavu; Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman na naibu wake ni Khamis Juma Mwalim.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Haji Omar Kheri na naibu wake ni Shamata Shaame Khamis.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed na naibu wake ni, Mihayo Juma Nhunga; Waziri wa Afya, Hamad Rashid Mohamed na naibu wake ni Harusi Said Suleiman.

Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati, Salama Aboud Talib na naibu wake ni Juma Makungu Juma;

Waziri wa Biashara na Viwanda, Balozi Amina Salim Ali na naibu wake ni Hassan Khamis Hafidh; Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma na naibu wake ni Mmanga Mjengo Mjawiri.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Khalid Salum Mohamed; Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Mahmoud Thabit Kombo na naibu wake ni Choum Kombo Khamis; Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto ni Maudline Cyrus Castico na naibu wake ni Shadia Mohamed Suleiman. Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Rashid Ali Juma na naibu wake ni Dk Makame Ali Ussi.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Dk Sira Ubwa Mamboya na naibu wake ni Mohamed Ahmada Salum; Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Balozi Ali Abeid Karume na naibu wake ni Lulu Msham Abdulla.

Katika uteuzi huo, Said Soud Said na Juma Ali Khatib wameendelea kuwa wajumbe wa Baraza la Mapinduzi na mawaziri wasiokuwa na wizara maalum.

Wakati huo huo; Dk Shein amefanya uteuzi na kuwabadilisha nafasi baadhi ya viongozi katika taasisi mbalimbali za Serikali, wakiwamo wakuu wa wilaya, makatibu tawala wa mikoa na wilaya na ofisa mdhamini wa Wizara ya Afya (Pemba).