Martha Karua azuiwa kuingia Uganda, aamriwa kuondoka
Mwanasiasa mashuhuri na Waziri wa zamani wa Sheria wa Kenya, Martha Karua
Mamlaka za usalama nchini Uganda zimemzuia kuingia nchini humo mwanasiasa mashuhuri na Waziri wa zamani wa Sheria wa Kenya, Martha Karua, na kuamuru arejee mara moja jijini Nairobi.
Tukio hilo la kushtua limefichuliwa na Chama cha Wanasheria cha Uganda (ULS), likiongeza joto la kidiplomasia na kiusalama ndani ya Ukanda wa Afrika Mashariki (EAC).
Karua alikuwa ametua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe leo kujiunga na jopo la mawakili wanaomtetea wakili mwenzao wa Uganda, Erias Lukwago.
Wawili hao wamekuwa wakimwakilisha kiongozi mkuu wa upinzani nchini Uganda, Dk Kizza Besigye, anayekabiliwa na mashtaka ya uhaini.
Taarifa rasmi kutoka ofisi ya Martha Karua imethibitisha kuwa mwanasiasa huyo alizuiliwa kwa muda uwanjani hapo na mawasiliano yake yote kukatwa.
"Timu yake ya wasaidizi waandamizi inaripoti kuwa hapatikani kabisa, simu zake zote za mkononi zimezimwa na bado tunasubiri mawasiliano ya moja kwa moja kujua hali yake na muda atakaorejea," ilieleza taarifa hiyo iliyotolewa leo Jumatatu, Juni 22, 2026.
Licha ya Karua kuzuiliwa, Rais wa Chama cha Wanasheria nchini Kenya (LSK), Charles Kanjama, aliyesafiri naye, aliruhusiwa kuingia Uganda bila kipingamizi.
Kanjama ameonyesha masikitiko makubwa kupitia mtandao wa X: "Inasikitisha na ni vigumu kuelewa kwa nini mjumbe mmoja wa jopo la utetezi anaruhusiwa kuingia nchini wakati mwingine anafukuzwa, ilhali wote wamesafiri kwa ajili ya jambo moja na kwa uwezo uleule wa kitaluma."
Wakili Lukwago alikamatwa nyumbani kwake na kufikishwa mahakamani Jumatano iliyopita.
Lukwago anashtakiwa kwa kosa la kushindwa kutoa taarifa za uhaini zinazohusiana na kesi ya Besigye, mashtaka ambayo aliyakana na kunyimwa dhamana hadi Jumatatu ya leo.
Dk Kizza Besigye amekuwa gerezani tangu alipotekwa akiwa jijini Nairobi, Kenya, na kurudishwa kwa nguvu nchini Uganda mwishoni mwa mwaka 2024, tukio lililoibua mjadala mzito wa kikanda kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu na mipaka ya kisheria.
Mwaka jana, Martha Karua alifukuzwa na kurejeshwa kwao (deported) na mamlaka za Tanzania ili kumzuia kuhudhuria na kuingia mahakamani kumtetea Makamu Mwenyekiti wa chama cha upinzani cha Chadema, Tundu Lissu, ambaye pia anakabiliwa na mashtaka yanayohusiana na uhaini.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wanasheria cha Afrika Mashariki (EALS), Wakili Ramadhan Abubakar Mukira, amelaani hatua ya mamlaka za Uganda kumzuia na kumfukuza nchini humo mwanasheria mwandamizi na Waziri wa zamani wa Sheria wa Kenya, Martha Karua.
Katika tamko lake la dharura lililotolewa leo Jumatatu (Juni 22, 2026), Mukira ameeleza kuwa kitendo hicho ni ukiukwaji mkubwa wa haki za kisheria na kinahatarisha juhudi za utangamano wa kikanda na uhuru wa wanasheria kufanya kazi nje ya mipaka ya nchi zao (cross-border legal practice).
Mukira amesisitiza kuwa EALS haitanyamazia hatua yoyote inayokandamiza tasnia ya sheria.
Amesema kuzuiliwa kwa Karua, ambaye alikuwa na kibali halali cha uwakilishi wa kisheria nchini Uganda kilichotolewa na Baraza la Sheria la nchi hiyo, kunakiuka Mkataba wa Kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Treaty) na Itifaki ya Soko la Pamoja inayoruhusu uhuru wa kutembea kwa wataalamu.
Taasisi hiyo imetangaza kuwa inafanya mapitio ya kisheria ili kuwasilisha malalamiko rasmi katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) ili kupinga tabia ya nchi wanachama kuweka vizingiti vya kisiasa kwa mawakili wa kikanda.
Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.