Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waziri wa Nishati Kenya azuiwa kuingia bandarini

Waziri wa Nishati nchini Kenya, Charles Keter      

Muktasari:

Uamuzi huo wa Rais Magufuli umeizindua Kenya ambayo Rais wake, Uhuru Kenyatta amefufua mazungumzo na Rais Yoweri Museveni wa Uganda akimhakikishia usalama wa bomba hilo na kutochelewesha malipo ya fidia kwa watakaochukuliwa ardhi kwa ajili ya kupisha mradi huo.

Tanga. Bomba la mafuta linalojengwa kati ya Uganda na Tanzania limezidi kuivuruga Kenya baada ya waziri wake wa nishati na makatibu wakuu wawili kuzuiwa kuingia kwenye msafara wa viongozi wa Uganda wa kutembelea Bandari ya Tanga.

Awali, mradi huo wa bomba la mafuta linalotazamiwa kujengwa kuanzia Hoima, Uganda hadi Bandari ya Tanga, ulilenga kuishia Lamu nchini Kenya, lakini matatizo ya kiusalama na malipo ya fidia kwa wamiliki wa ardhi ulifanya uhamishiwe Tanzania baada ya Rais John Magufuli kuonyesha utayari.

Uamuzi huo wa Rais Magufuli umeizindua Kenya ambayo Rais wake, Uhuru Kenyatta amefufua mazungumzo na Rais Yoweri Museveni wa Uganda akimhakikishia usalama wa bomba hilo na kutochelewesha malipo ya fidia kwa watakaochukuliwa ardhi kwa ajili ya kupisha mradi huo.

Museveni na Kenyatta walikutana Jumatatu lakini hawakufikia muafaka na kukubaliana kukutana ndani ya wiki mbili, huku mawaziri wa nishati wa nchi hizo mbili wakipewa jukumu la kuwasilisha mpango wa pamoja wa ujenzi wa bomba hilo na gharama za usafirishaji.

Lakini waziri huyo wa Kenya, Charles Keter akiwa na ujumbe wake, walizuiwa kuingia kwenye msafara wa Uganda uliotembelea Bandari ya Tanga kwa kuwa hakukuwepo na taarifa zao, gazeti la Daily Nation liliripoti.

Alikuwa ameongoza na katibu mkuu anayehusika na mafuta, Andrew Kamau na mwenzake wa nishati, Joseph Njoroge pamoja na mtendaji mkuu wa mradi wa reli inayotoka Mombasa hadi Sudan Kusini, Sylvester Kasuku.

Awali, maofisa hao walitembelea eneo la Lamu ambako taarifa ya utafiti uliofanywa na kampuni tatu za mafuta zinaonyesha kuwa bado hakuna bandari iliyojengwa na kwamba ujenzi wake unaweza usikamilike kabla ya 2018, mwaka ambao Uganda imepanga kuanza kusafirisha nje mafuta.

Gazeti hilo lilisema kuwa hati za kusafiria za maofisa hao wa Kenya zilizuiwa wakati wakitaka kujiunga na msafara huo wa Uganda.

Gazeti hilo lilisema kukamatwa kwao ni kujibu mapigo baada ya Kenya kutoialika Tanzania katika ujumbe uliotembelea Bandari ya Lamu na katika mazungumzo yaliyofanyika Ikulu ya Nairobi baina ya Rais Kenyatta na Museveni.

Kamau aliithibitishia Daily Nation kuwa hati hizo zilishikiliwa mjini Tanga.

“Walikataa kuturejeshea pasipoti zetu kwa karibu saa nzima. Pia, wametukatalia kuingia Bandari ya Tanga. Wameruhusu tu ujumbe kutoka Uganda,” alisema Kamau.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo jana, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela alisema ujumbe wa Kenya ulizuiwa Uwanja wa Ndege kwa kuwa hakukuwapo na taarifa za kuwasili kwao.

“Ukweli ni kwamba Serikali ya Tanzania ilikuwa na taarifa za ujio wa Waziri wa Maendeleo ya Nishati na Madini wa Uganda, Irene Mulono kwa ajili ya kutembelea Bandari ya Tanga na kukagua sehemu litakapoanzia bomba la mafuta, ndiyo maana tukaenda uwanja wa ndege kumpokea,” alisema Shigela.

Alisema lakini walishangaa kumuona waziri huyo wa Kenya na ujumbe wake katika msafara wa Uganda.

“Kwa kawaida kiongozi kama huyo anapowasili nchi nyingine, ni lazima atawasiliana na ama katibu mkuu mwenzake au waziri, lakini hakufanya hivyo. Sisi kazi yetu ni kuwapokea na kuwapeleka wanakohitaji, lakini waziri huyu hakufanya hivyo,” alisema.

Ujumbe wa mawaziri hao uliwasili kwa helkopta nne na kwa pamoja ulikuwa na watu 20 wakiwamo maofisa 13 kutoka Kenya, saba kutoka Uganda pamoja na viongozi wa kampuni za mafuta za Tullow ya Ubelgiji, CNOOC ya China na Total ya Ufaransa.

Ziara bandarini

Baada ya sakata hilo, waziri wa Uganda alitembelea bandarini ambako Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), James Mataragio alieleza uzoefu wa Tanzania katika ujenzi, ulinzi na utumiaji wa mabomba ya mafuta tangu mwaka 1968 lilipojengwa bomba la Tazama kati ya Dar es Salaam na Zambia.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justine Mtalikwa ambaye alimwakilisha waziri wake, Profesa Sospeter Muhongo aliuhakikishia ujumbe wa Uganda kwamba baada ya Rais Magufuli na Museveni kusaini makubaliano ya ujenzi wa bomba hilo, Tanzania ilianza maandalizi.

Naye Waziri Muloni alieleza kufurahishwa na mazingira aliyoyakuta na kubainisha kwamba ni tofauti na alivyokuwa akifikiria na kuahidi kutuma wataalamu kukagua kila mahali.