Kaka wa Lissu ahoji kwa nini polisi isimfuate dereva Nairobi

Muktasari:

  • Alute amehoji inawezekana vipi polisi wasimamishe shughuli kwa sababu ya mtu mmoja

Dar es Salaam. Kaka wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Alute Mughwai amehoji kitendo cha polisi kutokumfuata dereva wa Lissu jijini Nairobi badala yake wanamsubiri Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Alute amehoji inawezekana vipi polisi wasimamishe shughuli kwa sababu ya mtu mmoja. "Tunashauri polisi wapeleke mpelelezi kule wakachukue maelezo yake badala ya kusubiri arudi,"
Alute amesema hayo baada ya jana Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro amesema wanaendelea na upelelezi wa tukio la kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu.
IGP Sirro akizungumza akiwa ziarani mkoani Mtwara amemtaka dereva wa Lissu kulisaidia jeshi hilo katika kukamilisha upelelezi.
Lissu ambaye anapata matibabu katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya, alishambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi Septemba 7 nyumbani kwake Area D mjini Dodoma na watu wasiojulikana.
Amesema miongoni mwa wanaohitajika kwa kuhojiwa ni dereva wa Lissu ambaye inaelezwa yuko Nairobi anakopatiwa matibabu ya kisaikolojia.
Soma: Familia ya Lissu yafanya kikao na Bunge
“Yule kijana kwenye picha ukimwona yuko vizuri tu, sasa wanaposema anapata huduma ya kisaikolojia wakati kwenye magazeti anaonekana hii inatupa changamoto. Ndugu zangu, mheshimiwa Lissu amepigwa risasi na watu tunaowatafuta, huyo kijana aje. Kuja kwake kutatusaidia kupata majibu ya mambo mengi,” amesema IGP Sirro.
Amesema, “Mtu anasema anatibiwa kisaikolojia lakini kila siku nikiona magazeti anaonekana anawaka, inanipa tabu.”
IGP Sirro amewataka waandishi wa habari kuwasilisha taarifa hiyo kwa umma akisema, “Kimsingi waandishi wa habari naomba mlipeleke hili sisi tuna uchungu sana na mheshimiwa Tundu Lissu, tunamheshimu ni mtu muhimu kwa Watanzania na sisi tunataka tuwapate waliofanya lile tukio lakini ushirikiano ni mzuri ili  kufanikiwa,” amesema.