Fatma Karume kuchuana na watatu urais TLS

Fatma Karume

Muktasari:

  • Kwa sasa rais wa TLS ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ambaye yupo nchini Ubelgiji kwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30, Septemba 7 mwaka jana.

Dar es Salaam. Wanasheria wanne akiwamo Fatma Karume wamepitishwa na Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kuwania urais wa chama hicho katika uchaguzi utakaofanyika Aprili 14.

Kwa sasa rais wa TLS ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ambaye yupo nchini Ubelgiji kwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30, Septemba 7 mwaka jana.

Taarifa iliyotolewa jana na mwenyekiti wa kamati hiyo yenye wajumbe watano, Dk Kibuta Ongwamuhana iliwataja wagombea wa nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo utakaofanyika jijini Arusha. Wengine waliopitishwa kuwania nafasi hiyo ni makamu rais wa sasa, Godwin Ngwilimi, Godwin Mwapongo na Godfrey Wasonga huku Rugemeleza Nshalla akipitishwa kuwania umakamu wa rais.

Uchaguzi huo utafanyika huku Lissu aliyepaswa kuwapo ili kutoa taarifa ya utendaji ya mwaka mmoja, akiwa kwenye matibabu. Shambulio hilo limemfanya kutumikia nafasi hiyo kwa miezi sita.

Akizungumzia hatua ya uteuzi, Fatma alisema: “Siwezi kusema kwa sasa nitafanyaje kampeni lakini nawaachia wajumbe wa mkutano. Nikishinda nitahakikisha TLS inasimamia haki, utawala bora, kuheshimu misingi ya demokrasia na inayowajibika kweli.”