Fedha zakwamisha shughuli za Wizara ya Ujenzi

Katibu Mkuu wa wizara Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano , Dk Maria Sasabo 

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Maria Sasabo amesema zinahitajika juhudi za makusudi ili kupata fedha zitakazowezesha shughuli zilizopangwa kutekelezwa kikamilifu

Dodoma. Baadhi ya shughuli zilizopangwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano zimeshindwa kukamilika kutokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha za miradi ya maendeleo na matumizi mengineyo kwa wakati.

Akizungumza leo Machi 6, 2018 katika mkutano wa baraza la wafanyakazi wa sekta ya mawasiliano, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Maria Sasabo amesema zinahitajika juhudi za makusudi ili kupata fedha zitakazowezesha shughuli zilizopangwa kutekelezwa kikamilifu.

“Upatikanaji wa fedha za miradi ya maendeleo na matumizi mengineyo kwa wakati imekuwa ni changamoto ya kutokamilika kwa baadhi ya shughuli zilizopangwa,”amesema.

Aidha, amewahimiza wafanyakazi wa sekta hiyo kutoa elimu juu ya mawasiliano endelevu kwa umma ili kuelewa umuhimu wa sekta hiyo.

“Wafanyakazi watoe elimu ili wale ambao wanatumia vibaya mawasiliano kwasababu hawafahamu waweze kufahamu na kuwa na matumizi endelevu,”amesema.

Mwanasheria wa Sekta ya Mawasiliano, Yunis Masigati ametoa rai kwa wananchi kuwa makini na taarifa wanazopokea kutoka makundi mbalimbali ya mtandao na kuogopa kuzisambaza kwa watu.

“Tuna sheria ya makosa ya mtandao ya 2015 ambayo inaelekeza mtu yeyote kwa nia ovu anapoamua kutuma taarifa za uongo, kwa makusudi kwa nia ya kudanganya anakuwa ametenda kosa, katika kipindi hiki tumeona kuna makosa mbalimbali ya kimtandao ya kijamii, ninatoa rai kwa wananchi waweze kuwa makini,” amesema.