Gari alilopewa Kinana lazua mjadala

Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Abdulrahman Kinana akibidhiwa gari aina ya VOX alilopewa zawadi na wabunge wa chama hicho katika hafla ya kumuaga iliyofanyika, jijini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Kinana amepewa gari aina ya VOXY na wabunge wa CCM ambalo baadhi ya watu wanadai si hadhi yake.


Dar es Salaam. Gari aina ya VOXY aliyozawadiwa na wabunge aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana limezua mjadala kwenye mitandao ya kijamii baadhi ya watu wakieleza si la hadhi yake wengine wakisema fedha hizo zingetumika kutatua matatizo ya kijamii.

Mjadala umeibuka kwenye mtandao wa Facebook kutokana na habari picha iliyowekwa ukurasa wa gazeti hili ikionyesha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Kinana ufunguo wa gari hiyo kama zawadi ya wabunge wa chama hicho walipomfanyia sherehe ya kumuaga jijini Dodoma Juni 19 mwaka huu.

Maoni ya wachangiaji wengi yalionyesha kubeza thamani ya zawadi aliyopatiwa mtendaji huyo mstaafu wa chama tawala huku wengine wakisema ni bora fedha zilizotumika kununua zawadi hiyo zingetumika katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii.

Mtumiaji wa Facebook aliyejiandikisha kwa jina la Wilbroad Kwidika alikosoa akisema “Voxy Kinana ana peleka wapi. sisiem kuweni serious basi” aliungwa mkono na Peter Rambau aliyeandika hivi “Alishazoea kutembelea VX  mnampa ka-VOXy? mnataka afe kwa msongo wa mawazo”.

Watu waliendelea kutoa ya moyoni ni Nel Nyangalima alitumia msemo wa kiswahili usemao wenye nacho huongezewa kwa madai kuwa Kinana magari yamejaa nyumbani kwake lakini ameongezewa jingine wakati huo yeye hata usafiri wa baiskeli na akamaliza kwa kuandika kuwa ‘Life is not fair’.

Erasto Mgaya aliandika kuwa “Wanafunzi wamekosa nafasi za kujiunga na Kidato cha Tano kisa madarasa hakuna na mabweni lakini Leo mnagawana mtonyo kichama zaidi, Watanzania tuhurumiane” lakini Abdy alimjibu kwa kuhoji “Kazawadiwa na chama chake hii si pesa ya serikali sasa tatizo liko wapi?

Mann Zengwe yeye alikuja na hoja tofauti akisema fedha zilizotumika kununua zawadi hiyo na kuandaa sherehe zingeweza kutatua changamoto za kijamii. “Hizo pesa zingeweza kutumika kununua madawa, kujenga maabara, zahanati, miundo mbinu na kununulia vitabu vya shule kwa kila mwanafunzi. Lakini pia ingeweza kuwanufaisha wakulima na vijana wangepewa mtaji”.