Saturday, August 12, 2017

Gari la DC Chemba lapigwa mawe

 

By Sharon Sauwa, Mwananchi ssauwa@mwananchi.co.tz

Dodoma. Gari la Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga limeharibiwa kwa mawe baada ya wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Kambiyansa wilayani humo kulishambulia na kulivunja kioo alipokuwa akisafiri kuelekea mjini Dodoma.

Gari hilo la Odunga aliyekuwa na waandishi habari wakitokea Wilaya ya Kondoa kwa ajili ya shughuli za kijamii, lilishambuliwa na wanafunzi watatu waliokuwa wakitoka shuleni ambao walikimbia na kujificha katika nyumba ya jirani.

“Niliita askari wafanye msako wa harakaharaka kuwatambua watoto waliofanya vitendo hivyo na walifanikiwa kumkamata mmoja tu lakini wengine walijificha,” alisema na kuongeza kuwa askari waliwakamata wazazi wa watoto waliojificha ili iwe rahisi kuwakamata.

“Hii si mara ya kwanza kwa matukio kama haya, yameshawahi kujitokeza tena huko nyuma nina matukio kama matatu katika kijiji hiki ya watu kurushiwa mchanga au kupigwa mawe,” alisema.

Alisema vitendo hivyo vinaifanya Serikali itoe elimu kwa wakazi hao ili kujua matumizi ya barabara na kulinda amani kwa sababu inatumiwa na magari mengi tangu ilipokamilika.

Februari mwaka huu, Odunga aliwatandika viboko wanafunzi wa Sekondari ya Msakwalo walioandamana usiku wa manane kwenda ofisini kwake wakidai huduma za maji, muuguzi na kurejeshwa kwa ratiba ya kula nyama.

-->