Giza lamkuta Lukuvi akipambana na migogoro ya ardhi

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akizungumza na wakazi wa eneo la Malabi mjini Tabora jana. Picha na Robert Kakwesi

Muktasari:

  • Akiwa katika ziara ya kutatua migogoro ya ardhi juzi mjini Tabora, Lukuvi alipokea malalamiko kutoka kwa wananchi 541 katika Uwanja wa Chipukizi na kuyasikiliza huku mengine akilazimika kuyatolea maagizo na ufafanuzi hadi giza lilipoingia.

Tabora. Siku nne baada ya kuhitimisha ziara yake mkoani Mara alikokutana na zaidi ya watu 1,000 waliolalamika migogoro ya ardhi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amelazimika kutatua migogoro ya aina hiyo hadi usiku mjini hapa.

Akiwa katika ziara ya kutatua migogoro ya ardhi juzi mjini Tabora, Lukuvi alipokea malalamiko kutoka kwa wananchi 541 katika Uwanja wa Chipukizi na kuyasikiliza huku mengine akilazimika kuyatolea maagizo na ufafanuzi hadi giza lilipoingia.

Waziri huyo yupo katika ziara ya kushughulikia migogoro ya ardhi kwa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyefanya ziara mkoani hapa kati ya Agosti 16 hadi 18.

Katika ziara hiyo, Majaliwa alionyeshwa mabango na wananchi waliolalamikia migogoro ya ardhi na aliwaahidi kuwa Waziri wa Ardhi angefika kuishughulikia.

Aanza na migogoro 400

Awali, Lukuvi alielezwa kuwapo kwa zaidi ya migogoro 400 iliyoandikishwa katika Manispaa ya Tabora kuanzia Julai hadi Agosti.

Mwanasheria kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Richard Lugomela alimwambia waziri huyo katika kikao kilichomkutanisha na viongozi mbalimbali kuwa migogoro mingine imesababishwa na watendaji na madalali wa viwanja.

Alisema kuna migogoro ya aina tatu ikiwamo ile inayoshirikisha vijiji na maeneo ya hifadhi, vijiji na wananchi na ya wananchi na kambi za jeshi au taasisi za Serikali.

Pia alisema mabaraza ya ardhi yanalalamikiwa na wananchi kutoshughulikia ipasavyo migogoro.

Lugomela alisema migogoro 423 inahusisha wananchi kutolipwa fidia au kutoridhishwa na fidia waliyolipwa. Hata hivyo, ofisa huyo alisema tayari mkakati umewekwa ili kuishughulikia kikamilifu kuanzia mwezi ujao kwa lengo la kuhakikisha inafikia hatua nzuri.

DC ajiandaa kuwatumbua

Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Erick Komanya alimhakikishia Lukuvi kuwa kabla hajafika Dar es Salaam atasikia jambo kuhusu watendaji waliosababisha migogoro ya ardhi wilayani humo.

Alisema wapo baadhi yao walidiriki kukata maeneo ya shule na wananchi wanalalamikia utendaji wao kutoridhisha.

Komanya, ambaye tangu ameapishwa amekuwa akiwabana watendaji hasa maofisa ardhi kuhusiana na migogoro ya ardhi alisema kero zote atazifanyia kazi na waliohusika watachukuliwa hatua.

Aagiza hati zitolewe haraka

Akizungumza na wakazi wa manispaa hiyo, Waziri Lukuvi aliagiza wananchi 938 ambao viwanja vyao vimepimwa eneo la Malabi wapatiwe hati zao mara moja.

Lukuvi alisema haiwezekani eneo lipimwe zaidi ya miaka mitatu, lakini wananchi hawajapatiwa hati. “Huu ni uhujumu uchumi, haiwezekani,” alisema.

Alisema kitendo cha kutotolewa kwa hati muda wote huo ina maana Serikali imepoteza mapato ambayo yangetokana na kodi na uwekezaji.

Lukuvi aliwataka wananchi watakaolipia hati zao kuanza ujenzi huku akitoa miezi mitatu watu kujipanga kulipia na baada ya muda kwisha watakaoshindwa viwanja vyao watapewa watu wengine.

Waziri Lukuvi alisema uamuzi huo ni wa Serikali na kuwataka wanaopinga waende mahakamani.

Alisema mgogoro wa eneo hilo ni wa muda mrefu na hauwezi kuachwa uendelee bila kutafutiwa ufumbuzi, huku akiagiza wenye maeneo ambayo yana migogoro kwenda katika ofisi ya mkuu wa wilaya ili wasaidiwe.

Akizungumzia madai ya baadhi ya watu kuwa kuna wengine hawapo kwenye orodha ya ugawaji maeneo, lakini wameanza kujenga makazi, Lukuvi aliagiza nyumba hizo zibomolewe mara moja.

Mkuu wa wilaya, Komanya alisema kuna ujanja unafanywa katika ugawaji maeneo kwenye eneo hilo akiwatupia lawama watendaji na maofisa ardhi. Katika eneo la Malabi kuna viwanja 1,154 huku 1,137 vikiwa vya makazi na 17 vya matumizi ya umma.