Grayson Semsekwa, Ommy, Lauryn Hill walivyoteswa na tatizo la koo

Muktasari:

Rapa wa zamani wa bendi za Extra Bongo, Twanga Pepeta, na Chipololo, Grayson Semsekwa ameeleza alivyolazimika kukaa benchi baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa koo kwa miaka mitano


Ommy Dimpoz alianza taratibu kulalamikia kushindwa kumeza chakula na vimiminika. Ilifika wakati tonge la chakula alilisukumiza kwa maji akiamini ni tatizo tu la kawaida.

Miaka akakatika ndipo alipoamua kutafuta tiba ambayo sasa anaipata nchini Afrika Kusini. Kwa mashabiki wake ni habari ya kushtua lakini kumbe tatizo hili siyo geni miongoni mwa wasanii.

Rapa wa zamani wa bendi za Extra Bongo, Twanga Pepeta, na Chipololo, Grayson Semsekwa ameeleza alivyolazimika kukaa benchi baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa koo kwa miaka mitano.

Semsekwa ambaye kwa sasa amehamia mkoani Morogoro akiitumikia bendi ya Tamba Stars, amesema kuwa alifanyiwa upasuaji wa koo baada ya kugundulika kuwa ana uvimbe katika koo upande wa kushoto uliokuwa unamsababishia kushindwa kula, kumeza kimiminika chochote na kuimba kwa muda mrefu akiwa stejini.

Anasema alifanyiwa upasuaji na kupewa masharti ya kukaa mwaka mzima bila ya kufanya kazi ya muziki, kunywa pombe, kutovuta sigara na kutoshiriki tendo la ndoa.

“Sitasahau ugonjwa wa koo uliokuwa ukinisumbua, nilikuwa nashindwa kula, kumeza mate na kuimba kwa muda mrefu nikiwa stejini, nilipoenda Hospitali niliambiwa nina uvimbe kwenye koo upande wa kushoto hivyo natakiwa nifanyiwe upasuaji. Walianza kunichoma sindano ya kuivisha ule uivimbe na baadaye nikafanyiwa upasuaji, nilipewa masharti, ila kwa sasa naendelea vizuri na nina uwezo wa kuimba hata saa tatu bila ya kupumzika na sauti yangu imekuwa ni nzuri zaidi ya mwanzo,” anasema Semsekwa

Semsekwa ni Rapa Mkongwe ambaye aliwahi kutamba na rap kama ‘Kichaa kapewa Rungu….usijaribu kupita mbele yake” ,”Si sahizi usimuige kasuku kuongea” na nyingine nyingi.

Mchambuzi na mwanamuziki John Kitime anasema wasanii wengi wamewahi kupata tatizo hilo na wengine waliacha kabisa kujishughulisha na muziki akimtaja Linda Ronstadt wa Marekani.

Wengine anawataja kuwa ni Mariah Carey na Lauryn Hill aliyewahi kutamba na kundi la The Fugees.

Semsekwa alirudi kwenye muziki?

Semsekwa anasema baada ya kuona kapona alirudi katika kazi yake ya muziki na alipitia bendi nyingi hasa za mikoa na hadi alipofikia Tamba Stars kwa sasa.

“Nilipojiona nimepona nikaamua kurudi katika muziki,ambapo nilianzia katika bendi ya Chipolopolo lakini sikukaa sana,nikaondoka kwenda bendi ya TOT hapa nilikaa miaka miwili nikahama kwenda Extra Bongo na baada ya hapo nikatoka nikaenda Manyoni kulikuwa na bendi inaitwa Watanzo hapo nilikaa miaka miwili,lakini mfadhili alipofiwa, ilibidi niende kujiunga na bendi ya Sky Melodies iliyopo Dodoma hapa nilikaa mwaka mmoja na nusu

“baada ya hapo nikaenda kuanzisha bendi Songea ilikuwa inaitwa Peramiho nilidumu nayo kwa mwaka mmoja, nikaachana nayo nikarudi tena Sky Melodies nikakaa miezi sita,baada ha hapo niliamua kukaa nyumbani na kuanza kutoa nyimbo zangu kivyangu hadi nilipoamua kujiunga na Tamba Stars ya Morogoro sasa hivi, ”