CCM Singida Kaskazini kupiga kura ya maoni leo

Muktasari:

Gulamali alishinda kura ya maoni kabla ya CCM kusitisha mchakato na amezuiwa kugombea.

Singida. Haider Gulamali (46), aliyewania kuteuliwa kugombea ubunge Singida Kaskazini kwa tiketi ya CCM amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Singida.

Gulamali aliyesomewa mashtaka mbele ya Hakimu Flora Ndale jana Jumatano Desemba 13,2017 anasubiri uamuzi wa mahakama kuhusu dhamana.

Baada ya kusomewa mashtaka jana alipelekwa rumande kutokana na mvutano wa kisheria kati ya mwanasheria wa Takukuru, Edson Mapalala na wakili wa mshitakiwa, Godfrey Wasonga kuhusu dhamana.

Gulamali aliyeshinda kura ya maoni kabla ya CCM kusitisha mchakato amezuiwa kugombea nafasi hiyo akituhumiwa kwa rushwa.

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alitumia mamlaka yake kuitisha upya mchakato wa kumpata mgombea wa chama hicho na uchaguzi unafanyika leo Alhamisi Desemba 14,2017 na utafunguliwa na Kinana.