H’shauri kuboresha machinjio yaliyokimbiza wawekezaji

Hali ya machinjio ya sasa ambayo yalijengwa enzi za ukoloni. Picha na Rehema Matowo

Muktasari:

Huenda yakavutia wawekezaji kununua nyama Geita

Geita. Uwapo wa miradi mbalimbali ya uwekezaji hasa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), ulifikiriwa ungeinua uchumi wa wafugaji, kwa kununua nyama inayozalishwa mjini hapa.

Hata hivyo, hali hiyo ni tofauti kutokana na uongozi wa GGM kutoridhishwa na kiwango cha usafi wa machinjio yanayotumika kuandaa nyama hiyo.

Ikiwa ni miaka mitano tangu kuanzishwa kwake mwaka 2012, Mkoa wa Geita bado unatumia machinjio yaliyojengwa enzi za ukoloni.

Kutokana na kupanuka kwa mji na ongezeko la watu wanaokadiriwa kufika 300,000, Halmashauri ya mji wa Geita imeanza ujenzi wa machinjio ya kisasa eneo la Mpomvu utakaogharimu Sh2.7 bilioni kwa awamu ya kwanza.

Akizungumza ofisini kwake juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Modest Apolnary alisema awamu ya kwanza ambayo ni ujenzi wa machinjio hayo ni msaada kutoka Benki ya Dunia (WB) unatarajiwa kukamilika Mei mwakani.

Kuhusu mradi huo, wafanyabiashara wa nyama mjini hapa walisema baada ya machinjio hayo kukamilika yatakuwa mkombozi kutokana na yaliyopo sasa kujengwa kipindi cha mkoloni.

Usafi ni kikwazo

Katibu wa wachinjaji, Nchembi Joseph alisema mazingira yasiyokidhi viwango vya usafi yalisababisha kukosa biashara baada ya Kampuni ya Kuchimba Dhahabu Geita (GGM) kukubali kununua nyama katika machinjio hayo, lakini walibadili uamuzi kutokana na uchafu.

Pia, alisema kutokana na machinjio hayo kuwa kwenye makazi ya watu wamekuwa wakipata malalamiko ya uwapo wa harufu mbaya eneo hilo na kusababisha migogoro.

Naye Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Ramadhan Mitenengo alisema licha ya machinjio yaliyopo kutoendana na mazingira ya sasa ya afya, ni finyu na husababisha kuwapo msongamano wa wachinjaji. “Haya machinjio yalijengwa kwa ajili ya kuchinja ng’ombe saba kwa siku, sasa tunachinja zaidi ya ng’ombe 30 kwa siku na sikukuu wanafika hadi 60 imebidi tuweke zamu maana watu watakatana mikono,” alisema.

Mitenengo alisema hulipa ushuru wa Sh5,000 kwa ng’ombe na kwamba, machinjio mapya huenda yakapunguza ajira kwa sababu kwa sasa ng’ombe mmoja huchinjwa na watu wanne.