Hoja 20 zilizojadiliwa na Kamati ya Uongozi ya Bunge kuanikwa

Muktasari:

  • Hoja hizo ni kati ya 23 zilizowasilishwa kwa Kamati ya Uongozi inayoongozwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai na Kamati ya Bajeti iliyozijadili kuanzia Juni 6, baada ya kumalizika kwa bajeti za kisekta za wizara.

Dodoma. Kikao cha 52 cha mkutano wa Kumi na Moja wa Bunge kinaendelea leo kwa wabunge kuanza mjadala wa bajeti ya Serikali ya mwaka 2018/19, huku mbivu na mbichi za hoja 20 zilizowasilishwa kwa Kamati ya Uongozi zikitarajiwa kujulikana.

Hoja hizo ni kati ya 23 zilizowasilishwa kwa Kamati ya Uongozi inayoongozwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai na Kamati ya Bajeti iliyozijadili kuanzia Juni 6, baada ya kumalizika kwa bajeti za kisekta za wizara.

Juni 13, Kamati ya Uongozi ilikutana na watendaji wa Serikali wakiwamo kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kujadili hoja hizo zilizowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Hawa Ghasia.

Akizungumza kabla ya kuingia katika kikao hicho, Ghasia ambaye pia mbunge wa Mtwara Vijijini (CCM) alisema walipoanza mjadala Juni 6, walikuwa na hoja 23 lakini waliafikiana hoja tatu.

Ni matarajio kwamba leo Kamati ya Bajeti itaeleza kipi ambacho waliafikiana walipozipeleka hoja kwa Kamati ya Uongozi.

Ghasia aliyekuwa kikaoni akifanya maandalizi kuandaa taarifa ya kamati jana, alidokeza kuwa hoja hizo ni sehemu ya taarifa itakayosomwa bungeni leo.

Baada ya taarifa ya Kamati ya Bajeti kusomwa, itafuata hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Hotuba hiyo ambayo ni bajeti mbadala itasomwa na Naibu Msemaji wa Wizara ya Fedha na Mipango, David Silinde.

Kambi hiyo juzi ilibainisha vipaumbele vitano vya bajeti mbadala ambavyo wangevitekeleza iwapo wangekuwa madarakani.

Silinde atasoma hotuba kwa niaba ya msemaji wa wizara hiyo, mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee ambaye atakuwa mahakamani jijini Dar es Salaam kuhudhuria kesi inayomkabili pamoja na viongozi wengine wa chama hicho wakiongozwa na mwenyekiti, Freeman Mbowe.

Akizungumza jana, Silinde ambaye ni mbunge wa Momba (Chadema), alisema watavijadili kwa kina vipaumbele hivyo na kutoa bajeti mbadala isiyozidi Sh27 trilioni na kuonyesha wapi fedha sitapatikana.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi jijini Dodoma, Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni elimu; kilimo, mifugo na uvuvi; viwanda katika mnyororo wa thamani wa kilimo; afya na maji; na utawala bora.

Baada ya Kamati ya Bajeti na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kumaliza kuwasilisha taarifa; wabunge wataanza kujadili taarifa hizo pamoja na Bajeti ya Serikali ya mwaka 2018/19 ya Sh32.47 trilioni iliyowasilishwa Juni 14 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango.

Mjadala huo utakuwa wa siku saba kuanzia leo hadi Juni 26 itakapopigwa kura kuipitisha au kutoipitisha bajeti.

Pia, watajadili taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2018/19.

Mbowe katika mkutano na waandishi wa habari juzi alisema kumekuwa na kauli za mara kwa mara kwamba Serikali inajenga uchumi wa viwanda ikitolewa na mawaziri na hata wabunge lakini kwenye bajeti hakuna mkakati wowote wa Serikali kwenda kwa uchumi wa viwanda.

Alisema hakuna mazingira yoyote yanayoweza kukuza uwekezaji kama hakuna utawala bora na kwamba utawala bora ni usimamizi wa sheria na Katiba.

Mbowe alisema katika mwaka wa fedha 2016/17, Serikali ilipanga kukusanya Sh29.54 trilioni lakini iliweza kukusanya mapato kutoka vyanzo vyote yaliyofikia Sh20.7 trilioni sawa na asilimia 70.1 ya lengo, ikiwa na maana kuwa asilimia takriban 30 iliyobaki (sawa na Sh8.83 trilioni) ilikuwa ni makusanyo hewa.

Alisema katika mwaka huu wa fedha 2017/18 unaoelekea mwishoni, Serikali ilipanga kukusanya Sh31.71 trilioni lakini imekusanya Sh21.89 trilioni sawa na asilimia 69 ya lengo.

“Hii ina maana kwamba asilimia 31 iliyobaki (sawa na Sh9.82 trilioni) ilikuwa ni hewa,” alisema Mbowe.