Huduma ya afya kutoka meli ya Wachina yakumbwa na ‘vikwazo’

Madaktari kutoka China wakimsaidia mmoja wa watu waliyojitokeza kupima afya zao kuingia katika meli ya ‘Ark of Peace’ katika Bandari ya Dar es Salaam jana kwa ajili ya kutoa huduma za upimaji wa magonjwa mbalimbali bure. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Huduma hiyo inatolewa bandarini Dar es Salaam katika meli ya Wachina iliyotia nanga kwa ajili ya kufanya vipimo na matibabu bure kwa wananchi.

       Dar es Salaam. Maelfu ya wananchi waliojitokeza jana kupima afya zao kwa madaktari bingwa kutoka China ulifanya zoezi hilo kuonekana gumu kutokana wananchi wenyewe kushindwa kufuata utaratibu ili waweze kupata huduma hiyo.

Huduma hiyo inatolewa bandarini Dar es Salaam katika meli ya Wachina iliyotia nanga kwa ajili ya kufanya vipimo na matibabu bure kwa wananchi.

Kuanzia asubuhi jana gazeti lilishuhudia baadhi ya mamia ya wagonjwa wakiwa kwenye foleni huku wagonjwa wengine wakiwa wanagombana kwa ajili ya kupatiwa namba.

Hata hivyo baadhi ya wananchi hao walisema vurugu hizo zilitokea kutokana na baadhi yao kutotaka kukaa kwenye mstari.

Wagonjwa mahututi walikuwa wakilalamikia kitendo cha baadhi ya watu kuingia ndani na kuchukua kadi nyingi na kisha kuanza kuziuza jambo ambalo ni kinyume na taarifa iliyotolewa awali kwamba matibabu katika meli hiyo ni bure.

Habiba Hassan ambaye ni Mkazi wa Temeke yeye alielezea kuwa kitendo cha vijana kuchukua kadi yenye namba za kumuwezesha mgonjwa kwenda kupata vipimo kimesababisha wagonjwa wengi wenye uhitaji wa matibabu ya haraka kushindwa kupata huduma hiyo. “Vijana ndiyo wanaopewa namba, wakina mama ambao tuna wagonjwa wenye uhitaji mkubwa hatupewe hizo namba, hivi kweli mgonjwa anaweza akawa anakimbilia namba? Alihoji Habiba

Pamoja na hayo Habiba ametoa wito kwa Serikali kuweka utaratibu bora utakaozingatia mahitaji ya mtu kulingana na hali yake na si kila mgonjwa ambaye mwingine utakuta anaumwa malaria akawa anaenda mahali hapo kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Ismail Juma alisema amewahi tangu saa 11 asubuhi lakini amekaa kituoni hapo bila ya kupatiwa namba huku akidai kuwa wamekuwa na upendeleo katika zoezi hilo.

“Nimekuja mapema lakini bado sijapewa namba haiwezekani watoe kwa kujuana,” alisema Juma.

Awali namba hizo zilikuwa zinatolewa na Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Grace Magembe hata hivyo alishindwa kutokana na kusongwa na wagonjwa wengi ambao walikuwa hawataki kufuata utaratibu waliopangiwa

Hata hivyo, Dk Magembe alishindwa kuendelea na utaratibu huo na kuwaachia polisi wagawe namba hizo.

Hata walipoachiwa polisi bado vurugu za kung’ang’ania namba pamoja na kwamba walitengeneza utaratibu wa kugawa namba kwa makundi.

Polisi na baadhi ya wahudumu wa afya waliendelea na utaratibu huo huku wananchi wengi wakiendelea kumiminika.

Pamoja na kufurika kwa wananchi hao Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva amewataka waendelee kujitokeza kwa wingi kupima afya zao kwa kutumia madaktari hao bingwa kutoka China.

Akizungumza jana na waandishi wa Habari alisema madaktari hao wameingia juzi kwa ajili ya zoezi la upimaji wa afya bure hivyo wananchi wanatakiwa wajitokeze kwa wingi.

“Meli hii ni ya Wachina hivyo matibabu yanatolewa kwenye meli hiyo bandarini kwa kufuata utaratibu wa kupatiwa namba,” alisema Lyaniva.

Alisema zoezi hilo halichagui hivyo wananchi wa maeneo yote wanaruhusiwa kupimwa bure na kupatiwa matibabu.

Lyaniva alisema kabla ya kwenda bandarini mgonjwa atalazimika nje ya makao makuu ya trafiki kwa ajili ya kupatiwa namba hivyo ukiwamaliza unapanda gari kwenda bandarini kutibiwa. Alisema kwa siku madaktari hao wamekusudia kuhudumiwa wagonjwa 600.

Matibabu ndani ya meli

Akizungumzia hali ya ndani ya meli mara baada ya kupatiwa matibabu mgonjwa Asha Kahamba ambaye ni mkazi wa Mbagala akiwa na matatizo ya mgongo na moyo wake kuwa mkubwa, ameeleza hajaridhishwa na huduma inayotolewa na madaktari hao kutoka China.

Alisema aliwasili eneo la kuchukulia kadi saa kumi na moja asubuhi na kupewa kadi namba 21 lakini alichokikuta ndani ya meli hiyo ni kukosekana kwa mawasiliano kati ya madakrari Watanzania na hao wa kutoka China.

“Mimi sijui kuzungumza kizungu wala kichina, mkalimani kutoka China hajui Kiswahili sasa hii inatufanya tushindwe kujieleza, lakini kama madaktari wetu wa hapa nchini wangeshirikishwa ipasavyo na kuwa karibu na hao wa China zoezi la kutusikiliza lingekuwa rahisi,” alisema Kahamba.

Alisema pamoja na kwamba yeye anatibiwa katika Hospitali ya TMJ bado alipopima afya yake ameonekana kuwa hana tatizo lolote isipokuwa ana tatizo dogo upande wa mgongo.

“Mimi ninaumwa mgongo hadi nashindwa kutembea, lakini pia moyo wangu umekuwa mkubwa na unajaa maji wao wanasema nina tatizo dogo, hili jambo limenishangaza na kunifikirisha sana,” alisema Kahamba.