ISM yatoa ufadhili kwa wanafunzi wanane nje

Muktasari:

Mkurugenzi Mtendaji wa ISM, Bob Horton alisema kwa ufadhili wa mwaka huu unafanya thamani ya jumla ya walionufaika ndani ya miaka mitano iliyopita kuwa Dola milioni nane za Marekani (zaidi ya Sh38.72 bilioni).

Moshi. Shule ya Kimataifa ya International School Moshi (ISM), imewatafutia ufadhili wa zaidi ya Sh4.7 bilioni wanafunzi wanane kwenda kusoma nje ya nchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa ISM, Bob Horton alisema kwa ufadhili wa mwaka huu unafanya thamani ya jumla ya walionufaika ndani ya miaka mitano iliyopita kuwa Dola milioni nane za Marekani (zaidi ya Sh38.72 bilioni).

Wanafunzi hao watakwenda kusoma katika vyuo vikuu vilivyopo Marekani, Canada na Uingereza. “Mwaka huu tumepata ufadhili wa Dola 2.1 milioni za Marekani (zaidi ya Sh4.7 bilioni) kwa ajili ya wanafunzi wanane, watakaojiunga na vyuo vikuu bora duniani,” alisema Horton. Kozi zinazofundishwa na ISM zinawaandaa wanafunzi kuwa viongozi wa siku zijazo hasa kupitia progamu yake ya diploma ya kimataifa ya Baccalaureate (International Baccalaureate Diploma programme).

Mkurugenzi huyo alisema moja ya malengo ya ISM ni kuwasaidia watoto wenye uwezo wa kuwa viongozi katika nyanja mbalimbali kupata elimu bora kutoka vyuo vinavyotambulika kimataifa, hivyo inao mpango wa kutafuta ufadhili kwa wanafunzi wake.

Horton aliwataja waliobahatika kupata fursa hiyo kuwa ni Fatema Bhimani anayekwenda kusoma Chuo Kikuu cha Harvard; Angel Mcharo atakayekwenda Chuo Kikuu cha Duke, Elias Kalembo; Chuo Kikuu cha Yale, Lydia Nichols; Chuo Kikuu cha Washington vyote vya Marekani na Sakina Nazarali anayekwenda Chuo Kikuu cha Simon Fraser nchini Canada. Wengine ni Blaise Kramer atakayejiunga na Chuo Kikuu cha George Washington, Esuvat Bomani atakayekwenda Chuo Kikuu cha Cornell na Erik Ngoiya anayekwenda Chuo Kikuu cha Trinity, Marekani.