Ibada ya mazishi ya Pancho Latino yaanza Lugalo

Muktasari:

Anatarajia kuzikwa kesho nyumbani kwao Gairo, mkoani Morogoro


Dar es Salaam. Ibada ya mazishi ya mtayarishaji wa muziki nchini Joshua Magawa 'Pancho Latino', imeanza katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo.

Pancho alifariki dunia Oktoba 9, 2018 akiwa anapatiwa matibabu katika Zahanati ya Mtongani iliyopo Kunduchi jijini Dar es Salaam baada ya kuzama katika Kisiwa cha Mbudya alipokuwa akiogelea.

MCL Digital imeshuhudia watu mbalimbali wakiwemo ndugu, jamaa, marafiki na wasanii mbalimbali.

Baada ya shughuli ya kuaga mwili wa Pancho baadhi ya waombolezaji watasafiri kuelekea kijijini kwao Gairo katika eneo la Msingisi mkoani Morogoro kwa ajili ya maziko yatakayofanyika kesho.

Enzi za uhai wake, Pancho alijizolea umaarufu kwa kutengeneza midundo ya nyimbo mbalimbali zikiwemo za Dar es Salaam Stand Up (Chid Benz); Baby Candy wa Dully Sykes; Closer wa Vanessa na nyinginezo.

Pancho alizaliwa Mei 18,1988 na ni mtoto wa mwisho kati ya watoto tisa wa familia ya mzee Joshua Magawa.