Idara ya uhamiaji yatakiwa kudhibiti wahamiaji haramu

Muktasari:

Alisema inashangaza kuona silaha za aina nyingi katika maeneo mbalimbali ambazo Tanzania hakuna ambazo zinadaiwa kuingia nchini kupitia maeneo ya mpakani.

Arusha. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ameitaka Idara ya Uhamiaji kudhibiti wahamiaji haramu kwa kuanza kufanya misako katika nyumba za kulala wageni ili kuwabaini wageni wanaoingia nchini bila ya kibali kwani ni chanzo cha kuingiza silaha haramu nchini.

Waziri Mkuu aliyasema hayo leo (Ijumaa, Desemba 2, 2016) wakati akizungumza na walimu wa halmashauri ya Jiji la Arusha na wilaya ya Arusha kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya kikazi mkoani Arusha.

Alisema inashangaza kuona silaha za aina nyingi katika maeneo mbalimbali ambazo Tanzania hakuna ambazo zinadaiwa kuingia nchini kupitia maeneo ya mpakani.

 “Hivyo ni lazima Idara ya Uhamiaji ihakikishe wanadhibiti uingiaji wa wahamiaji kwenye mipaka mbalimbali nchini,”.

Waziri Mkuu amesema Serikali haizuii wageni kutoka mataifa mengine kuingia nchini ila ni lazima udhibiti wa wageni hao ufanyike ikiwa ni pamoja na kujiridhisha sababu za kuja nchini na muda watakao kuwepo.

Hata hivyo aliwasihi watumishi wa idara mbalimbali za Serikali kuhakikisha wanafanya kazi kwa nidhamu, weledi, uadilifu na kuwatumikia wananchi wanaohitaji huduma mbalimbali hata kama wamekosea kuuliza katika maeneo yao.

Alisema:

 “baadhi ya wananchi  hawana uelewa juu ya wapi wapeleke malalamiko yao lakini kwa kuwa wewe ni mtumishi wa umma unapaswa kumsikiliza na kumwelekeza aende wapi badala ya kumtolea maneno yasiyofaa.”.