Tuesday, February 13, 2018

JKCA: Afya pacha walioungana yaimarika

 

By Tumaini Msowoya, Mwananchi tmsowoya@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCA), Profesa Mohammed Janabi amesema afya za pacha walioungana Maria na Consolata  zinaendelea kutengemaa.

Akizungumza na MCL Digital leo Februari 13, 2018, Profesa Janabi amesema pacha hao waliokuwa kwenye chumba cha uangalizi maalumu (ICU) wameshatolewa na  wanaendelea vizuri na matibabu yao.

Maria na Consolata walilazwa katika taasisi hiyo Januari 2, 2018 baada ya kupewa rufaa kutoka katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa walikofikishwa wakisumbuliwa na matatizo ya moyo.

Tayari Rais John Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wameshakwenda kuwajulia hali pacha hao wanaoendelea kutibiwa chini ya jopo la madaktari  bingwa sita wanaoongozwa na Profesa Janabi.

Pacha hao ni kati ya walemavu waliofanikiwa kuonyesha uwezo wa kielimu tangu walipohitimu na kufaulu darasa la saba mwaka 2010 katika Shule ya Msingi ya Ikonda wilayani Makete na baadaye kidato cha nne katika Sekondari ya Udzungwa wilayani Kilolo.

Mwaka jana pacha hao wanaosoma Chuo Kikuu cha Katoliki cha Ruaha (Rucu) walifaulu mitihani yao ya kidato cha sita iliyowawezesha kuanza masomo ya ualimu chuoni hapo.

Kwa sasa Maria na Consolata wanalelewa na Serikali kwa kushirikiana na Rucu. Awali, walikuwa wakilelewa na Shirika la Masista la Maria Consolata.

 

 

 

 


-->