JPM, Museveni kuweka jiwe la msingi bomba la mafuta

Muktasari:

  • Urefu wa bomba hilo ni kilometa 1,445 na kati ya hizo kilometa 1,115 zinajengwa Tanzania.

Rais John Magufuli na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Agosti 5 mwaka huu wataweka jiwe la msingi la mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi la Afrika Mashariki.

Bomba hilo la mafuta ghafi litatoka Hoima, Uganda hadi Bandari ya Tanga, nchini.

Taarifa ilitotumwa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, imesema kuwa mradi huo ni miongoni mwa miradi mikubwa ambayo nchi yetu imeipata na kuanza kutekeleza tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani Novemba, 5, 2015.

“Ni mradi ambao uwekezaji wake ni mkubwa wa Dola za Marekani Bilioni 3.5 sawa na takribani Sh Trilioni 8,” imesema taarifa hiyo.

Urefu wa bomba hili ni kilometa 1,445 na kati ya hizo kilometa 1,115 zinajengwa Tanzania na mafuta ghafi yatakayosafirishwa ni mapipa 216,000 kwa siku.

“Nachukua fursa hii, kuwaalika Watanzania wote kufuatilia matangazo ya moja kwa moja yatakayorushwa na vituo vya redio, televisheni na mitandao ya kijamii kwa siku hiyo ya sherehe za uwekaji jiwe la msingi na pia kufuatilia matangazo mbalimbali na machapisho yatayotolewa na vyombo vyetu vya habari na mitandao ya kijamii kuelekea siku hiyo,” imesema taarifa hiyo.