JPM afungua fursa mbolea ya Minjingu

Muktasari:

  • Minjingu ni mbolea asilia ya kupandia.Mbolea hii inatokana na miamba inayochimbwa eneo la Minjingu mkoani Manyara ambayo husagwa na kufungashwa kwenye kiwanda hicho.

Ndoto ya uchumi wa viwanda kwa vitendo imeendelea kuonekana baada ya Rais John Magufuli kufungua milango mingine katika soko la mbolea inayozalishwa na Kiwanda cha Mbolea cha Minjingu, Minjingu Mines and Fertilizer Limited.

Minjingu ni mbolea asilia ya kupandia.Mbolea hii inatokana na miamba inayochimbwa eneo la Minjingu mkoani Manyara ambayo husagwa na kufungashwa kwenye kiwanda hicho.

Mbolea hiyo ina kirutubisho cha mimea aina ya fosiforasi kati ya asilimia 12.3 na 13.2. Tofauti na mbolea nyingine za kupandia zenye madini hayo kama vile TSP na DAP ambazo huagizwa nje ya nchi

Kirutubisho cha fosiforasi huimarisha mizizi wakati mimea inapokua, hivyo kuiwezesha kunyonya maji pamoja na virutubisho kwa wingi toka ardhini na kustahimili zaidi hali ya ukame. Mbolea hii huyeyuka taratibu hivyo kudumu muda mrefu katika udongo baada ya kuwekwa.

Rais Magufuli ameonyesha dhamira ya kutumika kwa viwanda vya ndani huku akikemea ‘figisu figisu’ zinazojitokeza katika soko la mbolea ya Minjingu.

Rais Magufuli anasema inashangaza mbolea hiyo kuonekana ikiuzwa nje ya nchi wakati hapa nchini inapigwa vita na kujengewa mazingira ya kuchukiwa na wakulima.

Kauli hiyo ameitoa hivi karibuni Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kupokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2016/17 iliyoibua madudu katika baadhi ya taasisi pamoja na mashirika ya umma.

“Palikuwa na ‘process’ ya kununua mbolea ya nje, wakati kwenye kiwanda cha hapa cha Minjingu hawataki kwenda kununua, wakati mbolea ya Minjingu inauzwa kwenye nchi nyingine, panatengenezwa maneno ya figisufigisu hivi, kwamba wakulima hawazihitaji wakati content ni zilezile tu,” alisema Rais Magufuli.

INAENDELEA UK 28

INATOKA UK 27

“Sasa kama mkulima haihitaji, akainunue yeye ile anayoihitaji, aifuate mwenyewe, lakini sisi ni lazima tutimize malengo yetu kwa kuangalia mbolea iliyo cheap (rahisi) kwa manufaa ya Taifa. Kwa hiyo ushauri mlioutoa hapa CAG ni wa manufaa makubwa.”

Mtendaji mkuu wa Mamlaka ya Mbolea Tanzania (TFRA), Lazaro Kitandu anasema kwamba mahitaji ya mbolea katika msimu wa mwaka 2017/18 ni tani 400,000. Mbolea ya kupandia ni wastani wa tani 150,000 na ile ya kukuzia ni tani 250,000.

Kitandu anasema zaidi ya asilimia 90 ya mbolea inaagizwa nje na kampuni za ndani chini ya usimamizi wa TFRA.

“Uwezo wa Minjingu kwa taarifa alizotuletea hadi sasa inaonyesha hawajawahi kuzalisha zaidi ya tani 20,000 kwa mwaka na wamekuwa wakisambaza wastani wa tani 3,000 za mbolea kwa mwaka,” anasema Kitandu ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya zabuni ya uagizaji mbolea.

Hata hivyo, mkurugenzi wa kiwanda cha Minjingu, Tosky Hans anasema wana uwezo wa kuzalisha tani 150,000 za mbolea ya kupandia na kukuzia kwa mwaka.

“Si kila mahali inakubalika mbolea ya Minjingu na si kwa kila zao. Yako mazao ambayo inasaidia. Wakulima wanalalamika kuwa haitoi matokeo ya papo kwa papo, lakini kama uwezo wake umefikia uwezo wa kuuza tani 25,000 nje, basi tunampongeza. Anachotakiwa ni kujitangaza kwa soko la ndani, pia awasiliane na wizara ili aweze kupata ushirikiano zaidi kwa sababu tunataka wazalishaji wa ndani wapate nafasi,” anasema Kitandu.

Mahitahi ya soko

Kwa mujibu wa TFRA, kiwango cha mbolea ya kupandia na kukuzia kilichotumika mwaka jana kilikuwa tani 215,000 tu. Mbolea zinazoagizwa kupitia Mfumo wa Uagizaji Pamoja wa Mbolea ni Urea na DAP ambazo ni maalum kwa kupandia na kukuzia mazao.

Katika taarifa ya hivi karibuni kupitia tovuti ya wizara hiyo ya Kilimo, Kitandu anasema mbolea ya Urea tani 20,000 ilitarajia kuingizwa Februari 18, 2018 kabla ya kuagiza tani 35,000 nyingine mwezi Machi.

Anasema ongezeko la matumizi ya mbolea kwa wakulima linatokana na punguzo kubwa la bei. Alisema matumizi ya mbolea hiyo yanatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 45 ifikapo mwisho wa msimu huu.

Kitandu anasema mwaka jana kulikuwa na tani 389,135, lakini mbolea iliyobaki nchini ilikuwa tani 215,000. Anasema kwa sasa zaidi ya asilimia 50 ya mbolea inayotumika hapa nchini ni ya kukuzia, Urea ikiongoza. Mbolea nyingine za kukuzia ni pamoja na CAN, SA, NPK.

Tahadhari na manufaa

Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Asasi za Kilimo (Ansaf), Audax Rukonge anasema uwezeshaji wa viwanda vya ndani ni jambo linalotakiwa kuungwa mkono.

Hata hivyo, Rukonge anasema uzalishaji wa mbolea hiyo unatakiwa kuzingatia mahitaji ya soko la ndani kulingana na mazingira. Anasema Minjingu haiwezi kuwa mwarobaini wa mahitaji ya ardhi yote nchini. Anasema kwa kawaida mbolea inakuwa na virutubisho mbalimbali vikiwamo Urea, Potassium, Calcium lakini mbolea ya Minjingu haina mchanganyiko huo.

“Kwa fursa hiyo ya Rais (John Magufuli), wazalishaji wa Minjingu wanatakiwa sasa kuongeza virutubisho zaidi katika mbolea hiyo ili iweze kuwa msaada kwa wakulima wa kila mkoa. Waje na ‘product’ tofauti ya mbolea iweze kutumika kulingana na asili ya ardhi ya kilimo,

Pili, Rukonge anasema kuna uwezekano pia wa kuwekeza katika mbolea za DAP zinazotumia gesi asilia kutokana na upatikanaji wa malighafi hizo. Hatua hiyo itapanua soko la mbolea hiyo katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, mhadhiri mwandamizi wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Haji Semboja anasema faida zinazopatikana kupitia uwezeshaji wa viwanda vya ndani ni pamoja na kukuza ajira za ndani, kuongeza pato la Taifa, kukuza fedha za kigeni na kurahisisha mazingira ya uchumi wa viwanda.

“Tutakuwa na manufaa hayo lakini sera ya uwezeshaji wa viwanda vya ndani unatakiwa kutosheleza kwanza soko la ndani kabla ya kuuza nje ya nchi, ajira, fedha za kigeni na uzalishaji utaongezeka,”anasema Profesa Semboja.

Uwezo wa Minjingu

Mbali na uwezo wa kuzalisha tani 150,000 kwa mwaka, Hans anasema mwaka jana waliuza nje tani 8,000 na mwaka huu tayari Kenya imeshahitaji tani 25,000 za mbolea hiyo.

Mbolea hiyo ya Minjingu hutegemea zaidi masoko ya wakulima wa Mikoa ya Kusini, Sumbawanga, Kigoma, Mpanda, Njombe, Ruvuma, Iringa, Morogoro huku ikiuza katika mataifa matatu ya Kenya, Uganda na Malawi.

Hata hivyo Hans anasema kiwanda hicho kina uwezo wa kutosheleza mahitaji ya soko la ndani kutokana na upatikanaji wa malighafi za kutosha hapa nchini na uwezo wa mitambo yake ya kuzalishia.

“Tunatumia malighafi ya madini yanayotokana na masalia ya mifupa ya viumbe vya kale, kama vile samaki na flamingo, ndiyo tunachimba na inapatikana tu, mitambo yetu ina uwezo wa kuzalisha mahitaji yote ya ndani,” anasema Hans.

“Tunajipanga kuonana na Wizara ya Kilimo kwa ajili ya kufanya mazungumzo yatakayosaidia kurahisisha hatua zote za usambaji wa mbolea hiyo kwa muda sahihi na bei nafuu kwa wakulima,”anasema Hans.

Kuhusu ubora, Hans anasema Taasisi za Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Uyole (ARI-Uyole), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Kenya (KARI) Taasisi ya Utafiti wa Kilimo cha Tobacco Tanzania (TORITA) na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Selian (SALI) zimethibitisha ubora wa Minjingu.

“Karibu taasisi zote za kilimo zimeithibitisha Minjingu. Kwa hiyo tulikuwa tunapigwa vita ya propaganda ya kibiashara tu, mwaka wa tatu huu tunapigwa vita lakini hatuna changamoto inayoweza kukwamisha,” anasema.