JPM amtwisha msalaba wa Magereza CGP Kasike

Muktasari:

Alionyesha kushangazwa na viongozi wa jeshi hilo kushindwa kuwatumia wafungwa kufyatua matofali ya kujengea makazi yao wakati kuna maeneo na udongo unaofaa.

Tangu Rais John Magufuli ameingia mada-rakani amekuwa akilinyooshea kidole Jeshi la Magereza kutokana na kero mbalimbali alizoona zinalirejesha nyuma.

Kutokana na kuto-ridhishwa kwake na utendaji wa jeshi hilo, Rais Magufuli amekuwa akitoa maagizo kwa vion-gozi wa jeshi hilo tangu alipoingia madarakani Novemba 2015 wakati jeshi hilo likiongozwa na Kamishna Jenerali Casmir Minja aliyestaafu Desemba 2, 2016.Baada ya kustaafu kwa Minja, Rais Magufuli alimteua Dk Juma Malewa kukaimu nafasi hiyo kabla ya kuthibitishwa miezi mitano iliyopita.Hata hivyo, Kamishna Jenerali, Malewa amestaafu hivi karibu na sasa nafasi yake imechukuliwa na Phaustine Kasike.

Akizung-umza baada ya kumuapisha Kamishna Jenerali Kasike, Rais Magufuli amemtwisha mambo muhimu anayotaka yarekebishwe, huku akimpa pole na hongera kidogo.Jambo la kwanza alilotaja ni kutopandishwa vyeo kwa maofisa wa jeshi hilo.“Kwanza si siri, Jeshi la Magereza, askari wamekaa kama wameachwa hivi. Hata katika promosheni zao, imekuwa tatizo.

Wakati nam-promote kamshna Jenerali aliyestaafu, pali-kuwa na makamishna wawili tu,” anasema Rais Magufuli.Anasema si kwamba maofisa hao hawana sifa, kiasi kwamba hata wakati wa kumteua Kasike ilikuwa kazi ngumu. “Si kwamba askari magereza hawana sifa, wapo wazuri sana, lakini walikuwa wameachwa tu.

Wameachwa ama kwa makusudi au kwa kuogopa wale wali-otangulia pale juu. Ukishakuwa na jeshi kama hilo, performance (utendaji) inakuwa chini,” anasema.Amempongeza kamishna Jenerali mstaafu akisema wakati anaingia kulikuwa na maka-mishna wawili lakini hadi anastaafu walifikia 10.

Alimtaka Kamishna mpya kuendeleza hatua hizo.Jambo la pili alilolitaja ni jeshi hilo kutege-mea bajeti ya Serikali kulisha wafungwa wakati wanaweza kuwatumia kuzalisha chakula.

“Ni aibu kwa nchi kuendelea kulisha wafungwa. Maeneo ya magereza ni mengi mno. Ukienda kule Mbeya, mashamba yanalimwa nafikiri robo tu. Kila mahali kuna Magereza na maeneo mengi lakini kila mwaka kuna maombi ya bajeti kwa ajili ya kulisha wafungwa,” anasema na kuongeza:

“Definition (tafsiri) ya kufungwa maana yake ukamenyeke kazi na askari Magereza kazi yao ni kuwawezesha wale wafungwa wakafanye kazi kweli kweli. Ndiyo maana wengine wanahukumiwa na mboko ili zimwezeshe kufanya kazi.”

Anaendelea: “Sasa unapokwenda kwenye gereza wafungwa hawafanyi kazi, panatokea ukuta au nyumba imebomoka, unamkuta Kamishna Jenerali anaomba fedha kwenda kununua matofali na kadhalika, ni kitendo cha aibu.”

“Hakuna sababu enzi za Nyerere, gereza kwa mfano la Kingolwira lilikuwa linazalisha mkonge, leo uzalishaji uko chini, wakati tunazungumzia viwanda na maeneo mengine mengi,” ameongeza.

Alionyesha kushangazwa na viongozi wa jeshi hilo kushindwa kuwatumia wafungwa kufyatua matofali ya kujengea makazi yao wakati kuna maeneo na udongo unaofaa.

“Unakuta watumishi na askari hawana nyumba za kukaa, wafungwa wanao, labor force ipo tena ya bure. Kumwambia tu fyatua matofali, akizubaa na teke unampiga, anafyatua, ili kusudi dhambi zake alizofanya uraiani azilipe vizuri,” anasema.

“Unakuta askari huna nyumba ya kulala, familia nyumba ya kulala, wafungwa wanalala kwenye nyumba, unawatafutia chakula kwenye bajeti ya Serikali. Hili kalisimamie,” ameongeza.

Kuhusu uteuzi wa maofisa magereza wa mikoa, Rais Magufuli ametaka kuwe na uteuzi unaozingatia sifa na weledi.

Mambo mengine aliyoyataja ni wafungwa wanaotumikia kifungo kukutwa na makosa mengine nje ya magereza.

“Sitaki niyasikie yale yaliyojitokeza Mbeya. Mfungwa amehukumiwa kufungwa, ni jambazi halafu anashikwa akiwa anawinda tembo anashirikiana kuua tembo porini na anashikiwa kule wakati kule amehukumiwa kufungwa,” anasema na kuongeza:

“Sitaki nisikie mfungwa aliyeacha familia yake kule nyumbani, anakuja mke wake kwenye gereza, anakaribishwa na askari wa magereza, akafanye mambo ambayo hakutakiwa kuyafanya akiwa gerezani.’

“Hakuna sababu ya mfungwa kuingia na simu wakati mnaweza kufunga kwenye mlango mashine ya ku-screen, itaonyesha tu kama ana kitu cha chuma hata kama amekimeza. Lakini vitu ambavyo ni muhimu kwa ajili ya ulinzi na usalama wa Magereza hamvitumii,” amesisitiza.

Ametaja pia suala la wafungwa kuwasiliana na jamaa zao kwa kutumia simu, huku akisema mtindo huo upo kwenye magereza ya Dar es Salaam.

“Sitaki kwenye magereza, wafungwa hawa, wakapate nguvu za kuvuta bangi na saa nyingine kujamiiana, ni kwa sababu hawafanyishwi kazi za kutosha,” anasema.

“Sitaki kusikia mfungwa afungwe, baadaye akiwa amefungwa kule akaanza kufuga mbuzi na ng’om,be anapeleka mpaka kwenye mnada anakuwa tajiri kuliko hata askari.”

Huku akimpa pole, Rais Magufuli amemtahadharisha Kasike kuwa atachukiwa na baadhi ya askari kwa hatua atakazochukua, lakini akamtaka kuzichukua kwa sababu badala yake atajikuta kwenye hatari ya kukosana naye.

“Nataka Magereza ikafanye kazi, nataka askari wangu wafaidike. Hakuna sababu Magereza wanakuwa hawana vitendea kazi kama matrekta wakati JKT walipokesha mpaka raia. Magereza wangekuwa wamekopa hayo matrekta ningekuwa nimeshasamehe yale madeni, lakini hawakukopa halafu wanalalamika hawana vitendea kazi,” anasema Rais Magufuli.

Ameongeza: “Sitaki nione Magereza, hata watoto wa askari magereza wana kwashiorkor wakati mnaweza kufuga ng’ombe pale na mna wachungaji wapo na wanawachunga bure.”

Amelitaka jeshi hilo kutumia fursa ya mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kuuza kokoto kutoka kwenye maeneo yake.

“Sioni kwa nini Magereza wakose hela wakati sasa hivi kuna mradi wa standard gauge ambapo zinahitajika kokoto za kutosha, wakati mashine zipo na wafungwa wapo wa kuponda kokoto.

“Sasa mkijipanga vizuri, Jeshi la Magereza litakuwa ni jeshi la mfano mkubwa kwa maendeleo ya nchi hii.”

Kuhusu tatizo la makazi kwa watumishi wa jeshi hilo, Rais Magufuli alishangazwa na kutokamilika kwa mradi wa nyumba alioutolea karibu Sh10 bilioni.

“Wafungwa wapo na pesa nikatoa. Mngeweza kuwatumia yale majengo yakaisha, wafanyakazi wakawa wanakaa ndani. Mngeweza kuanzisha mradi wa kujenga nyumba kila mahali, kila gereza, wafungwa wakawa wanafyatua matofali. Mkiona wafungwa wamepungua, wasafirisheni wenmine muwapeleke mahali fulani,” anasema.

Amemtaka Kamishna Jenerali Kasike kutembelea Magereza na miradi ya jeshi hilo na kushirikiana na makamishna na maofisa wa jeshi hilo ili kuboresha utendaji.

Amemtaka pia kushirikiana na majeshi mengine ili kutekeleza jukumu la ulinzi na usalama wa nchi.

“Mimi nakupongeza kidogo, pole ndiyo kubwa. Katembelee Magereza, maeneo mbalimbali. Makamishna wengine na makamanda, mkatoe ushirikiano mkubwa.

Amesema Serikali yake inatambua mchango unaotolewa na majeshi yote na kuwataka wakuu wa majeshi ya ulinzi na usalama kukutana mara kwa mara kupanga mikakati kwa ajili ya Taifa.

Awali, Kamishna Jenerali Kasike alimshukuru Rais Magufuli kwa uteuzi huo na kumuahidi kutekeleza wajibu wake kwa uaminifu.

Akizungumzia utumishi wake katika jeshi hilo, Kamishna Jenerali Mstaafu, Dk Juma Malewa amesema kazi hiyo ina changamoto kubwa.

“Kuna changamoto za aina mbili, kwanza za askari na pili wafungwa wenyewe. Sisi tumekabidhiwa wahalifu, kila siku wanakuja na mbinu mpya,” anasema na kuongeza:

“Kama alivyosema Rais Magufuli, ni kweli lakini na sisi tunashindana na hizo changamoto. Wahalifu wenyewe wamesoma wana uelewa mkubwa, kwa hiyo hata kukabiliana nao pia inahitaji nguvu kubwa.”

Akieleza utekelezaji wa mambo yaliyopewa na Rais, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola aliyeteuliwa Julai 2 alisema amejitahidi kuhakikisha kuwa anamaliza tatizo la ajali za mara kwa mara.

“Ulisema umechoka kutoa salamu za rambirambi. Kuna hatua zimechukuliwa na IGP, sasa utapata usingizi na salamu za pole zitapungua,” alisema Lugola.

Kuhusu mikataba mibovu, alisema aliitisha kikao na viongozi wa majeshi yaliyo chini ya wizara hiyo ambayo ni Polisi, Magereza na Idara ya Uhamiaji na kuwapa siku 21 kutafakari suala hilo.

“Hatuwezi kuwa na tuhuma za Watanzania zisizokwisha, nimeapa sitakuangusha, nitachukua hatua bila kuangalia mtu usoni,” alisema.

Kuhusu uteuzi wa Kamishna Jenerali Kasike alisema awali alimtabiria kufika mbali alipotembelea Chuo cha Urekebishaji Tanzania (TCTA) Ukonga Dar es Salaam, alichokuwa akikiongoza Kasike.