Rais Magufuli atoa maagizo Wizara ya Nishati, Rea

Muktasari:

Rais amewataka wakuu wa taasisi kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuiepusha Serikali na gharama

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameiagiza Wizara ya Nishati na Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) kuondoa changamoto za kawaunganishia nishati hiyo wananchi.

Pia, amewaagiza wakuu wa taasisi mbalimbali za umma kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuepuka gharama wanazoisababishia Serikali na kuchelewesha maendeleo kwa wananchi.

Hayo ameyasema leo Jumatatu Aprili 3, 2018 wakati akizindua kituo cha kufua umeme cha Kinyerezi II 240MV CCPP jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli amesema kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu gharama za kuunganishiwa umeme hivyo hatua za haraka zinahitajika kuchukuliwa.

"Wizara ya Nishati na Rea hakikisheni mnaongeza kasi ya kuunganishiwa umeme, yapo malalamiko machache machache ya wafanyakazi kuomba rushwa, yashughulikiwe hayo," amesema Rais Magufuli

Kuhusu malalamiko ya taasisi kucheleweshewa baadhi ya huduma amesema hilo linamkera na hataki kulisikia tena.

Amesema taasisi za Serikali zinatakiwa kufanya kazi kwa karibu hasa tunapotekeleza miradi mikubwa ya Taifa, tusicheleweshane.

"Mawaziri, wakurugenzi, wenyeviti wa bodi msiache kuwasiliana ninyi kwa ninyi, kama unaona unakwamishwa na taasisi nyingine, mambo kama haya nikisikia huwa yananiudhi, lugha ya mitaani yananiboa kweli kweli. Shirikianeni kwani mnawacheleweshea wananchi maendeleo," amesema Rais Magufuli.

Amesema kuwa umeme wa uhakika unachagiza kutekeleza Tanzania ya Viwanda kwani kwa sasa mahitaji ya nchi ni megawati karibu 1,40O lakini uzalishaji umefikia megawati 1515.3,"Bado tunahitaji umeme wa kutosha na tuongeze uzalishaji."