JPM awahakikishia ushirikiano wawekezaji kutoka nje

Rais John Magufuli

Muktasari:

  • Viongozi wengine waliokutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli leo, Jumanne ni Kaimu Balozi wa Uturuki nchini, Yunus Belet na Kaimu Balozi wa Jamhuri ya Korea Songwon Shin.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amewahakikishia wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Shirikisho la Taifa la Utengenezaji wa Mitambo ya Viwanda la China (CNMIF) kuwa Serikali yake itawapa ushirikiano katika mpango wao wa kuwekeza kwenye uzalishaji wa nishati ya umeme, viwanda na kilimo hapa nchini.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo, Jumanne Ikulu jijini hapa alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu Mwenyekiti wa CNMIF na Mbunge wa Bunge la Wananchi wa China, Zhan Xin.

Amesema Tanzania imejiwekea malengo ya kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka megawati kati ya 1,500 na 1,800 zinazozalishwa hivi sasa hadi kufikia megawati 10,000 na kwamba ili kufikia malengo hayo wawekezaji wanakaribishwa kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo vilivyopo kama vile gesi, makaa ya mawe na jua.

“Kwa hiyo Ndg. Zhang Xin kawaambie wawekezaji wenzako wa China waje Tanzania, nchini zetu ni ndugu na marafiki wa miaka mingi, itakuwa jambo jema wakija kuunga mkono juhudi zetu za kujenga viwanda kwa kuzalisha umeme mwingi na pia kushiriki katika miradi mingine ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu ya reli na barabara” amesema.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na Balozi wa Ufaransa nchini, Malika Berak ambapo viongozi hao wamezungumzia utekelezaji wa mambo mbalimbali ya ushirikiano pamoja na miradi ya maendeleo iliyotokana na makubaliano ya mkutano wa wafanyabishara wa Tanzania na Ufaransa uliofanyika hivi karibuni.