Waziri Jafo adai Polisi wanasababisha foleni ya magari hayo

Muktasari:

Waziri Jafo amedai kwamba foleni ya mabasi hayo sababu kubwa ni polisi  kusimama kwenye taa zake na badala ya kuacha mfumo mzima wa taa ufanye kazi yake

Dar es Salaam. Serikali imesema ni wakati mwafaka mabasi yaendayo haraka (Mwendokasi) kutumia mfumo wa  taa zilizopo katika barabara zake badala ya kuongozwa na askari wa barabarani.

Hatua hiyo hiyo itasasidia mabasi hayo kufika kituoni kwa wakati kuliko hivi sasa yanachelewa njia kutokana na kuongozwa na askari wa barabarani.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo baada ya kufanya ziara ya kutembelea mradi wa mabasi hayo kuanzia eneo la Morocco hadi Kivukoni.

Kutokana na hatua hiyo, Jafo amewagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka, Mhandisi Ronald Lwakatare   kuwasiliana na uongozi wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kuangalia uwezekano wa polisi kuacha kuyaongoza magari hayo.

Amesema taa za kuongozea magari zilizopo kwenye mfumo wa barabara za mabasi hayo ziachwe zifanye kazi ya kuongezea magari  badala ya askari.

 “Kuna umuhimu mkubwa wa mabasi haya yakatumia taa za barabarani kuliko kuongozwa na askari ili yaweze kukidhi mahitaji na malengo yaliyokusudiwa,’’ amesema Jafo.

Kuhusu mabasi ya  ‘Express’ yaliyotengwa maalumu kwa ajili ya  kutoa huduma ya moja kwa moja kutoka kituo kikuu cha Kivukoni  hadi  Kimara  na kutochukua abiria pindi yanaposhusha  yanaposhusha wasafiri  Kivukoni, hatua hiyo imekuwa  kero kwa  wanaotumia usafari huo hasa wanaotaka kwenda Kimara.

“Unaweza kukuta mabasi yanashusha abiria Kivukoni na kuna kundi la abiria wanaohitaji kwenda moja kwa moja Kimara, lakini hayachukui abiria, jambo hili linapaswa kurekebishwa kwani linasababisha kero kwa abiria,” amesema

Mbali na hilo,  amewataka madereva wa bodaboda  kutokukatisha katika  barabara za mfumo na  mabasi hayo  na kwamba kufanya hivyo ni  kuhatarisha usalama wao na abiria wanaotumia mfumo wa mabasi.