Jafo ataka shule za Serikali kutamba 10 bora kitaifa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani jafo.

Muktasari:

  • Ametoa kauli hiyo leo baada ya kutembelea shule ya sekondari Kibaha iliyopo mkoani Pwani

Pwani.  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo amewataka wakuu wa shule za sekondari za Serikali kuhakikisha mwaka 2019, shule hizo zinakuwa nyingi katika orodha ya shule 10 bora kitaifa.

Jafo ametoa kauli hiyo leo Jumapili Julai 15, 2018 alipotembelea shule ya sekondari Kibaha kutoa pongezi kwa walimu na wanafunzi baada ya shule hiyo kushika namba moja katika matokeo ya kitaifa ya kidato cha sita.

“Natoa wito kwa wakuu wa shule zote za sekondari za Serikali katika mwaka ujao wa masomo ni lazima wahakikishe shule 10 bora ziwe za Serikali. Hilo naamini linawezekana, kinachotakiwa kwa sasa ni kuongeza jitihada tu,” amesema Jafo.

Amesema baada ya Kibaha kushika nafasi ya kwanza, jambo hilo linapaswa kuendelezwa ili kulinda nafasi hiyo miaka ijayo.

“Kabla ya kufanyika kwa mtihani huu nilitembelea shule hii na kuzungumza na wanafunzi. Waliweka ahadi kuwa watafanya vizuri kwenye mitihani yao, ninashukuru wametekeleza ahadi hiyo. Wameleta heshima kwa mkoa na Taifa,” amesema.

Naye ofisa elimu wa Mkoa wa Pwani, Abdul Maulid amesema Serikali ina walimu wazuri, kinachotakiwa kufanyika ni usimamizi wa karibu.

“Nakuahidi waziri nimepokea maelekezo yako na kwa kushirikiana na watendaji wenzangu tutaendelea kusimamia elimu kikamilifu ili kuilinda nafasi hii,” amesema Maulid.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Kibaha, Chrisdom Ambilikile amesema mikakati waliojiwekea ni kuhakikisha wanafunzi wanaongeza bidii katika masomo, kujituma na kuwa na nidhamu.