Jaji Lubuva: Hatuna la kujifunza kutoka Kenya

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi, Jaji Lubuva aliyekuwa mwangalizi wa uchaguzi kupitia Jumuiya ya Madola amesema hata maamuzi yaliyotolewa na Mahakama ya Juu ya nchi hiyo ya kubatilisha matokeo ni ya kawaida na yangeweza kutolewa hata hapa nchini endapo Katiba na sheria zingekuwa zinaruhusu jambo hilo.

Mwenyekiti mstaafu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva amesema hakuna lolote jipya la kujifunza kutoka katika uchaguzi wa Kenya kwa mambo yaliyofanyika ni ya kawaida kulingana na mazingira ya katiba ya nchi hiyo.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi, Jaji Lubuva aliyekuwa mwangalizi wa uchaguzi kupitia Jumuiya ya Madola amesema hata maamuzi yaliyotolewa na Mahakama ya Juu ya nchi hiyo ya kubatilisha matokeo ni ya kawaida na yangeweza kutolewa hata hapa nchini endapo Katiba na sheria zingekuwa zinaruhusu jambo hilo.

“Yote hayo ni ya kawaida. Hatuwezi kusema Kenya ni role model (mfano wa kuigwa), wamefana hivyo kulingana na mazingira yao,” alisema.

Jaji Lubuva aliyekuwa anazungumzia kukerwa na kauli za baadhi ya Watanzania wakiwamo wanasheria, amesema si sahihi kusema kwamba hapa majaji au watendaji hawako huru kwa sababu wanateuliwa na Rais kwa kuwa wanafanya kazi zao kwa uhuru na wamewahi kufanya maamuzi makubwa ambayo ni kinyume na matakwa ya Serikali au chama tawala.

Ametolea mfano wa kesi ya uhaini Zanzibar ambayo mahakama ya Rufani ilihukumu na kuwaachia huru watuhumiwa, ikisema Zanzibar si nchi kamili.

Amesema kwa upande wa NEC kuna maamuzi mengi wamewahi kufanya na Rais au vyombo vya usalama havikuwaingilia.

Alipoulizwa vipi kitendo cha Rais kubadili watendaji wa Tume wakati au karibia na uchaguzi, amesema kuhusu kamishna aliyetuliwa kuwa Jaji yeye aliulizwa na kukubali kwa kuwa lilikuwa ni suala la mtu kupanda cheo.

“Hawa wengine wakiondolewa ni utaratibu tu, mbona hata huko Kenya wameondolewa wote kwenye Tume,” amehoji.

Akieleza ilikuwaje watazamaji wa uchaguzi Kenya waliona ulikuwa huru na haki, lakini Mahakama ya Juu inaona tofauti  , amesema kasoro zilizobainika zilikuwa za jikoni ambako watazamaji hawaingii, lakini kwa utendaji wa jumla mambo alikwenda vizuri.

“Hata hapa kwetu waangalizi huwa tunawaeleza wasiiingie jikoni. Tulipokuwa pale Kenya, Raila Odinga alikuja kulalamika tukamweleza taratibu tulizoona zimekwenda vizuri, lakini kama yako ya jikoni aende mahakamani. Alikwenda huko na akafanikiwa.

Mwanasheria huyo amesema jambo lililojitokeza katika uchaguzi huo wa Kenya ni kuwa viongozi na wagombea Afrika hawajawa tayari kukubali matokeo kwa kuwa hata baada ya Odinga kupinga na kushinda kesi, Rais Uhuru Kenyatta ameibuka na kuishutumu mahakama.