Wadhamini wa CUF wakwama mahakamani

Muktasari:

Jaji amesema ingawa wanajitambulisha kama bodi ya wadhamini wa CUF lakini malalamiko ni binafsi na si ya kitaasisi.   

Dar es Salaam. Jaji Wilfred Dyansobera wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, anayesikiliza kesi za migogoro ndani ya Chama cha Wananchi (CUF), amekataa kujiondoa kuziendesha.
Wajumbe wa bodi ya wadhamini wa CUF, kambi ya mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba waliwasilisha ombi kutaka Jaji Dyansobera ajiondoe kuendesha kesi.
Katika barua za kumtaka Jaji Dyansobera ajiondoe kwenye kesi, wajumbe hao walidai hawana imani naye kuwa atatendea haki kutokana na walichokiita mfululizo wa matukio ya upendeleo dhidi ya upande mwingine wa chama hicho.
Akitoa uamuzi leo Jumatano Desemba 13,2017 Jaji Dyansobera amesema baada ya kuchunguza kwa makini sababu na hoja za kumtaka ajiondoe amebaini hakuna jambo la kuonyesha alikuwa na upendeleo katika uendeshaji wa mashauri hayo.
“Hivyo maombi haya yanakataliwa. Yeyote ambaye hataridhika na uamuzi wangu, ana haki ya kukata rufaa,” amesema Jaji Dyansoebera na kuamuru kuendelea na usikilizwaji wa mashauri hayo.
Pia, amesema kwa mujibu wa sheria, vyama vya siasa huwa vinasajiliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na huwa na bodi ya wadhamini ambayo kwa mujibu wa sheria ya usajili ndiyo yenye mamlaka ya kushtaki na kushtakiwa.
Amesema baada kuangalia utambulisho wa walalamikaji katika mashauri, ingawa wanajitambulisha kama bodi ya wadhamini wa CUF, lakini malalamiko ni binafsi na si ya kitaasisi. “Hapa kuna walalamikaji 10 na malalamiko yao ni personal (binafsi). Hawa watu 10 si bodi.”
Jaji Dyansobera amesema jaji kujiondoa katika kesi huwa si jambo dogo kama ambavyo walalamikaji wanavyodhani, huku akisema kuwa msimamo wa kisheria na wa Mahakama ya Rufaa katika uamuzi wa kesi mbalimbali jaji anapopangiwa kesi anapaswa kusikiliza mpaka mwisho.
Amesema kwa mujibu wa ibara ya 107 (A) ya Katiba na kwa mujibu wa kiapo cha majaji, jaji anapaswa kutekeleza majukumu yake bila woga, upendeleo, huba, wala chuki na kwamba hapaswi kufuata shinikizo la vyombo vya habari uma wala mtu yeyote.
Jaji Dyansobera anasikiliza kesi zipatazo 13 za CUF zilizofunguliwa na bodi ya wadhamini wa chama hicho ya zamani, kambi ya Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.
Kesi nyingi zimefunguliwa dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Msajili, Profesa Lipumba na baadhi ya wanachama wakiwemo viongozi wanaomuunga mkono Profesa Lipumba na nyingine dhidi ya Profesa Lipumba na wenzake.
Wajumbe wapya wa bodi ya wadhamini wa chama hicho kambi ya Profesa Lipumba, waliosajiliwa hivi karibuni na Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (Rita), ilimwandikia barua Jaji Dyansobera ikimtaka ajiondoe katika kesi hizo.
Katika barua zao na hoja zilizotolewa na wakili wao, Mashaka Ngole, alidai wateja wake walifikia uamuzi huo kufuatia mfululizo wa matukio ya upendeleo kwa upande pinzani, kwa nyakati tofauti wakati wa uendeshaji wa mashauri hayo.