Jini mkata kamba lilivyomsumbua Werrason Bongo

Muktasari:

Hali ya sintofahamu ilianza baada ya baadhi ya wanamuziki wa Werrason kukosa hati za kusafiria

Kuna jambo unaweza kulifanya zaidi ya mara tatu hadi nne, lakini unajikuta unakumbwa na misukosuko ya hapa na pale mpaka kushindwa kulifanikisha.

Mmoja wa watu hao ni promota kutoka kampuni ya Chapakazi, Lengos VIP ambaye ndiye alikuwa mwandaaji wa onyesho la mwanamuziki kutoka nchini DRC, Werrason Ngiama Makanda.

Hali ya sintofahamu ilianza baada ya baadhi ya wanamuziki wa Werrason kukosa hati za kusafiria kwa wakati na kujikuta wanachelewa kuingia nchini siku ambayo onyesho lilikuwa lifanyike kwa kuwa nchi hiyo kama ilivyo Tanzania nayo ilikuwa imeingia katika mfumo wa kutoa hati kielektroniki.

Hata hivyo, uongozi huo wa Chapakazi uliokuwa umeandaa onyesho ukatoa taarifa ya kuliahirisha hadi Aprili 14, ambapo Werrason na wanamuziki wake ikabidi wakae Dar es Salaam kwa siku zote saba wakila bata huku wakisubiri siku hiyo ifike.

Hatimaye Aprili 14 ilifika huku eneo lililokuwa limetengwa kwa ajili ya shoo hiyo likiwa ni viwanja vya Escape One, ambapo kwa bahati mbaya hawakufikiria kuweka maturubai pamoja na hali ya mvua kuiona tangu mwanzo kwa kuwa ilikuwa ni kipindi cha masika.

Kutokana na hilo, waliahirisha shoo hiyo saa saba za usiku baada ya mvua kugoma kukatika, huku wakiwatangazia waliofika eneo hilo kutunza tiketi zao na riboni za mkononi kwa wale ambao walikuwa tayari wameingia katika viwanja hivyo.

Walifanya hivyo kwa maelezo kwamba shoo ingefanyika kesho yake katika ukumbi wa King Solomon, lakini siku ilipofika mambo yakawa yaleyale kwani katika ukumbi huo maji yalikuwa yamejaa mpaka barabara kubwa ya Ali Hassan Mwinyi, huku ukumbi ukiwa katikati ya maji.

Ikumbukwe kwamba Werrason kipindi hicho ilikuwa afanye maonyesho matatu kwa kuanza na Dar es Salaam, Mwanza na kisha Dodoma, lakini kote huku ilishindikana kutokana na hali ya hewa.

Hivyo mwisho wa siku mwandaaji ilibidi kutangaza kuahirisha maonyesho hayo mpaka Julai, ambapo moja lilifanyika Julai 6 katika viwanja vya Rocky City Mwanza, Julai 7 likafanyika Tripple ‘A’ huko Arusha na Julai 8 likamalizikia pale viwanja vya Maisha Live, Dar es Salaam.

Pamoja na nia hiyo nzuri, waandaaji walijikuta wakipata hasara baada ya mashabiki waliofika kuwa wachache tofauti na matarajio.

Mwaandaaji anasemaje?

Akizugumza na Mwananchi, Lengos VIP anasema aliyoyapitia ni mtihani kama ilivyo katika kazi nyingine na kuongeza kuwa yeye si wa kwanza kufikwa na mambo mazito kama hayo.

“Unajua mimi ni mfanyabiashara na kwenye kufanya biashara kuna kupata na kukosa, hali zote hizo unatakiwa uzikubali na ndiyo maana unaona pamoja na yote niliyoyapitia katika maandalizi ya shoo hii, bado nafsi yangu ina amani,” anasema VIP.

Alipoulizwa kwa nini hakuachana nayo kabisa pamoja na kukiri mara kwa mara kupata hasara baada ya kuahirisha maonyesho hayo mara tatu, mwandaaji huyo alisema kwamba alimrudisha Werrason kwa mara nyingine ili kulinda heshima yake ya kuaminiwa mbele za jamii.

Anasema kuwa awali wakati maonyesho hayo yalipoahirishwa, yalizungumzwa maneno mengi dhidi yake ikiwemo kuitwa tapeli, lakini alitaka kuwaonyesha Watanzania kuwa yeye si tapeli.

Pia anasema bado haijamkatisha tamaa katika kuendelea kuwaleta wasanii wengine na Desemba anatarajia kuwaleta wakubwa zaidi kati yao anaweza kuwa Fally Ipupa au Koffie Olomide kutoka DRC.

Serikali yafunguka

Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe anasema amefurahi kuona namna mwanamuziki huyo na kundi lake wanavyojituma jukwaani.

Dk Mwakyembe anasema alitegemea kuona wanamuziki wengi siku hiyo ili wajifunze namna wenzao wanavyofanya na kuwashauri kuwa wasiache kutumia fursa hizo kwa kuwa zitasaidia kuwainua kimuziki na kubadilishana uzoefu kwani mwanamuziki kama Werrason ni msanii wa siku nyingi na anajua mengi katika tasnia hiyo.

Naye Katibu wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania, Hassan Msumari anasema kuna mengi wamezungumza na msanii huyo tangu kuahirishwa kwa shoo zake hadi kufanyika.

Alisema ushauri ambao aliwapatia wataufanyia kazi ili muziki wa dansi urudi katika hadhi yake.

Msumari anasema moja ya mambo waliyoyagundua ni wasanii wa muziki huo kushindwa kutumia vilivyo mabadiliko ya teknolojia katika kuuendeleza na kubaki kulalamika kuwa chanzo cha kuyumba kwake ni kubaniwa kupigwa redioni na kuonyeshwa kwenye runinga, jambo ambalo kwa sasa watu walishalisahau.

Mashabiki watofautiana

Mwananchi lilizungumza na baadhi ya mashabiki jijini Dar es Salaam kutaka kujua walivyoiona shoo ya Werrason, ambapo walionekana kutofautiana.

Wapo waliosema iliwakuna kwani Werrason aliweza kucheza na mashabiki wake mwanzo mwisho na kupiga nyimbo ambazo walitamani kuzisikia akiwa anaziimba ‘laivu’.

Mmoja wa mashabiki hao aliyejitambulisha kwa jina la Anna Stanley, anasema msanii huyo amemkumbusha nyumbani kwao DRC ambapo alitoka huko miaka 30 iliyopita na kuwaomba waandaaji kuendelea kuwaletea wanamuziki wengine.

Juma Rehani anasema hakufurahishwa na shoo hiyo, kwani ilifanyika kwa muda mfupi tofauti na alivyofikiria kusuuzika zaidi.

“Yaani Werrason kapiga shoo saa tatu tu, kapanda saa nne kamaliza saa saba, watu tumetoka majumbani mwetu tunajua hapa mpaka kuche na angetuondoa hasira tulizokuwa nazo za kuahirishwa mara kwa mara kwa shoo yake, badala yake imekuwa ndivyo sivyo. Katuacha hapa yeye kaondoka zake huku bado tukiwa na hamu ya kupata burudani kutoka kwake,” anasema Juma.

Kwa upande wake, Naomi Issack anawataka watu waache kulalamika akisisitiza kuwa Werrason ameacha funzo kwa wasanii wengine wakubwa wanaokuja nchini ambao hupanda majukwaani saa nane usiku watu wakiwa wameshachoka kuwasubiri.

“Yaani alichokifanya Werrason kupanda jukwaani saa nne kimenikosha sana, wanamuziki wengine wakubwa wanaokuja hapa waige kutoka kwake, kwani katusaidia tumeburudika tukiwa bado hatujachoka na pia hakujali kwamba wamejitokeza watu wachache. Zaidi yeye alipiga kama uwanja umejaa, hivyo ndivyo inavyotakiwa wasanii wetu nao wajali mashabiki zao,” anasema.