Mtuhumiwa wa mauaji ya Monica aangua kilio kortini

Muktasari:

  • Joseph Irungu maarufu kama Jowie, alimwaga chozi huku mama yake akimkumbatia baada ya kuingia ndani ya chumba cha mahakama dakika chache kabla ya kesi kuanza kusikilizwa.
  • Upande mwingine mpenzi wake Jacque Maribe, alikuwa na baba yake Mwangi na mama pamoja na rafiki yao Dennis Itumbi kwa ajili ya kutoa msaada.

Nairobi, Kenya. Mtuhumiwa mkuu katika mauaji ya mfanyabiashara Monica Kimani leo asubuhi ameangua kilio mahakamani huku mama yake akimkumbatia kwa dakika kadhaa kabla ya kutoa maelezo.
Joseph Irungu maarufu kama Jowie, alimwaga chozi huku mama yake akimkumbatia baada ya kuingia ndani ya chumba cha mahakama dakika chache kabla ya kesi kuanza kusikilizwa.
Upande mwingine mpenzi wake Jacque Maribe, alikuwa na baba yake Mwangi na mama pamoja na rafiki yao Dennis Itumbi kwa ajili ya kutoa msaada.
Irungu na Maribe, watuhumiwa wawili katika mauaji hayo, walikataa kuhusika kumuua Kimani katika nyumba yake ya Lamuria Kilimani Septemba 19.
Maribe akiwa amevaa suti ya kijani na blauzi nyeupe alisema amekuja kufahamua mashtaka dhidi yake aliposomewa na Jaji Jessie Lesiit.
Waendesha mashtaka, wakiongozwa na Catherine Mwaniki, walisema watapinga watuhumiwa hao kuachiwa kwa dhamana kama alivyofanya mwanasheria anayewakilisha familia ya Kimani.
Mwaniki alisema baadhi ya mashahidi wanapaswa kuwekwa chini ya ulinzi wa ushahidi na kwamba bado walikuwa hawakamilisha upelelezi wao.
Maombi ya dhamana yao yatasikilizwa Jumatano ya Oktoba 17.