Jumuiya na Taasisi za Kiislamu watoa waraka wa Eid el -Fitr

Muktasari:

  • Waraka huo ulisomwa jana jioni na katibu wa jumuiya hiyo, Sheikh Ponda Issa Ponda katika Msikiti wa Mtambani uliopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania imetoa waraka wa salamu za Sikukuu ya Eid el-Fitr uliobeba mambo manane yakiwamo haki na uhai; uhuru wa habari na kujieleza, wa Bunge na Mahakama, wa kisiasa na Katiba Mpya.

Waraka huo ulisomwa jana jioni na katibu wa jumuiya hiyo, Sheikh Ponda Issa Ponda katika Msikiti wa Mtambani uliopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Waraka huo wenye kurasa tisa umesainiwa na kaimu mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Sheikh Shaaban Hijja Mrisho na Ponda kwa niaba ya masheikh na maimamu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu.

Sheikh Ponda alisema waraka huo unatokana na kikao cha jukwaa kongwe la jumuiya hiyo lililokutana Juni 14 kujadili masuala mbalimbali ya kidini na ya kijamii.

Huo ni waraka wa tatu kutolewa na taasisi za dini, ukitanguliwa na uliotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).

Baraza hilo Februari lilitoa ujumbe wa Kwaresima wa mwaka 2018 ambao ndani yake ulieleza msimamo wa maaskofu 35 na mbali ya masuala ya kiroho, pia yalihusu ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Machi 24, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), lilitoa waraka wa Pasaka ambao mbali ya masuala ya kiroho, ulitaja changamoto tatu na kuzifikisha kwa waumini.

Changamoto zilizotajwa katika waraka huo uliopewa jina la ‘Taifa Letu Amani Yetu’ na kusainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo nchini ni hali ya kijamii na kiuchumi, maisha ya siasa, na masuala mtambuka likiwamo suala la Katiba Mpya.

Jana, Sheikh Ponda akizungumzia suala la haki na uhai, alisema kwa siku za karibu kumekuwapo na matukio mabaya yakiwamo ya kuokotwa kwa miili ya watu kwenye fukwe za bahari na mito hali inayoashiria haki ya kuishi imeanza kutoweka.

“Jumuiya inaishauri Serikali ichukue hatua madhubuti za kurudisha amani ya wananchi na vyombo vya dola vinapaswa kulinda usalama wa wananchi. Ni wakati muafaka kwa tume ya kijaji kuchunguza masuala yote yanayohusu utekaji, kupotezwa na kuuawa watu,” alisema Ponda.

Akizungumzia haki na uhuru wa habari na kujieleza, alisema unaelekea kutoweka. Alisema kanuni za maudhui zinazoongoza na kusimamia uendeshaji wa sekta ya habari nchini zinatumika zaidi kuua uhuru wa kupata habari na kujieleza kwa wananchi.

Alisema viongozi wa jumuiya hiyo wanaishauri Serikali iwe na uvumilivu wa kusikia hata mambo isiyoyapenda.

“Jamii ina haki na uhuru wa kutoa maoni juu ya namna Serikali yao inavyofanya kazi zake, maoni hayo yanaweza kutumiwa na Serikali katika kuboresha utoaji huduma wake,” alisema.

Sheikh Ponda alisema jamii ina uhuru wa kusoma, kuangalia na kusikiliza maoni hayo ya ukosoaji kupitia vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Alisema kupunguza uhuru wa watu kujieleza na kupata habari si njia nzuri ya kuongoza Taifa.

Uhuru wa Bunge na Mahakama

Alisema imeshuhudiwa kubanwa na kupungua kabisa kwa uhuru wa Bunge, kwanza kwa kufutwa kwa haki ya wananchi kuona matangazo ya moja kwa moja ya wawakilishi wao wakiwa bungeni kama ambavyo ilizoeleka.

Sheikh Ponda alisema matendo kadhaa ya Bunge na Serikali yanapunguza hadhi na uzito wa mhimili wa Bunge kwa nchi.

Kiongozi huyo alisema kwa kiasi fulani uhuru wa mahakama nao umepungua, utendaji kazi wake na uwezo wake wa kujiendesha kifedha umewekwa mtegoni na Serikali, kwa kuwekewa masharti ya kumalizwa, kupelekwa kwa haraka au kutolewa kwanza hukumu za madai ya kikodi katika kesi zinazoihusisha Serikali.

Alisema jumuiya inaishauri Serikali ifuate Katiba na sheria na iache Bunge na Mahakama vijiendeshe na kufanya kazi zake kwa uhuru na kwa mujibu wa sheria na Katiba.

“Serikali haipaswi kutoa vitisho na maelekezo kwa mihimili hiyo ya nchi. Na pia ni muhimu fedha zinazopitishwa na Bunge kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za Mahakama zitolewe kama zilivyopangwa na zitolewe kwa wakati, bila masharti,” alisema.

Uhuru wa kuchaguana

Alisema imeshuhudiwa kukosekana kwa mazingira ya haki na uhuru wa kuchagua na kuchaguliwa katika chaguzi mbalimbali akidai inatokana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kutokuwa huru, na pia kuendesha na kusimamia chaguzi kwa misingi isiyo ya haki na usawa.

Sheikh Ponda alishauri Serikali, NEC, vyama vya upinzani na wadau wote kukaa pamoja na kujadili changamoto za mazingira ya uchaguzi ili kupata namna bora ya kuwa na chaguzi huru, za haki na zenye usawa.

Sheikh Ponda alizungumzia kukosekana kwa utii wa Katiba na sheria akidai umesababisha Serikali kutoheshimu mamlaka za Serikali za mitaa kwa kuziingilia na kupunguza uwezo wake wa kujitegemea kimapato.

Alisema jumuiya inaitaka Serikali kutii Katiba ya nchi kwa kuziacha mamlaka za Serikali za mitaa kufanya kazi zake kwa mujibu Sheria na ziachwe kuingiliwa na kusababisha kurudi nyuma katika shughuli za kimaendeleo.

Uendeshaji siasa

Sheikh Ponda alisema vyama vya upinzani nchini vimezuiwa kufanya mikutano ya hadhara, lakini viongozi wa chama tawala wamekuwa wakifanya mikutano bila kubughudhiwa.

“Tunaiomba Serikali iondoe zuio la mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya siasa. Pia Serikali ifanye kikao cha pamoja cha mashauriano ya kitaifa ambacho kitasimamiwa na viongozi wa dini ili kujadili changamoto za kisiasa nchini,” alisema.

Katika waraka huo, Sheikh Ponda aligusia suala la jamii na uchumi akiipongeza nia njema ya Serikali katika ukusanyaji wa kodi na usimamizi wa rasilimali za Taifa na kupinga rushwa, lakini akisema kumekuwa na malalamiko kwa walipa kodi hasa sekta binafsi namna mchakato huo unavyotekelezwa dhidi yao.

“Maeneo wanayolalamika ni mazingira kutokuwa rafiki katika ukusanyaji kodi, ukadiriaji kodi kuliko uwezo wa kibiashara wa walipa kodi, ubabe wa watoza kodi na kuwakomoa,” alisema Sheikh Ponda.

Aliishauri Serikali kukaa pamoja na wafanyabiashara na kuzungumza ili kuangalia namna ya kutatua changamoto hizo na kuboresha na uhusiano kati yao.

Kuhusu Katiba mpya, alisema ni wakati wa Serikali kurejesha mchakato huo ili kujenga msingi mpya wa utaratibu wa kisheria na kikatiba kwa Taifa.

Pia aliishauri Serikali kuitisha mkutano mkubwa wa kitaifa wa kikatiba ili kuweka misingi ya muafaka kati ya makundi mawili; lile linalokubaliana Katiba iliyopendekezwa na linalokubali rasimu ya Katiba ya Tume ya Jaji Warioba.

Alisema mkutano huo uhusishe uwakilishi mpana wa wananchi kutoka makundi mbalimbali ya kijamii, kuanzia viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, taasisi za dini, asasi za kiraia, makundi ya taaluma na vyama vya ushirika. Amir wa Shura ya Maimamu Tanzania, Sheikh Mussa Kundecha alisema waraka huo utasambazwa katika misikiti ili usome na Waislamu wapate ujumbe wa kilichoandikwa.