KESI MAUAJI YA LIBERATUS BARLOW: Maelezo yanayodaiwa ya Muganyizi yatoa ramani ya mauaji, safari Mwanza hadi Dar

Muktasari:

  • Akiongozwa na wakili wa Serikali, Robert Kidando mbele ya Jaji Sirilius Matupa, shahidi huyo D 4426 Sajenti Fred kutoka makao makuu ya upelelezi, Dar es Salaam aliiambia Mahakama kuwa mshtakiwa wa kwanza, Peter Muganyizi alikiri mbele yake wakati akimwandikisha maelezo kuwa ndiye aliyefyatua risasi iliyomuua Barlow.

Mwanza. Shahidi wa 21 katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Liberatus Barlow ameieleza Mahakama mshtakiwa alivyomueleza namna alivyompiga risasi kamanda huyo.

Akiongozwa na wakili wa Serikali, Robert Kidando mbele ya Jaji Sirilius Matupa, shahidi huyo D 4426 Sajenti Fred kutoka makao makuu ya upelelezi, Dar es Salaam aliiambia Mahakama kuwa mshtakiwa wa kwanza, Peter Muganyizi alikiri mbele yake wakati akimwandikisha maelezo kuwa ndiye aliyefyatua risasi iliyomuua Barlow.

Maelezo hayo yalionyesha historia ya mshtakiwa, kuanzia alipozaliwa, matukio mengine ya uhalifu aliyowahi kufanya kabla ya tukio hilo, jinsi alivyokutana na wenzake kupanga mbinu za kuvamia maeneo mbalimbali jijini Mwanza, Sirari na Dar es Salaam, vitu walivyopora na alivyotekeleza amri ya kupiga risasi na kuua.

Aliieleza Mahakama kuwa Oktoba 24, 2012 akiwa anafanya kazi Kituo cha Polisi Stakishari mkoani Ilala (mkoa wa kipolisi), alipigiwa simu na bosi wake Duan Nyanda na kumtaka kuripoti ofisini kwake haraka.

Alidai baada ya kufika alimkuta bosi wake akiwa na mtu ambaye alionekana kama ni mtuhumiwa maana alikuwa chini ya ulinzi.

Hivyo, Nyanda alimuagiza aandike maelezo ya onyo ya mtu huyo maana anatuhumiwa kumuua Barlow na alimtambulisha kuwa anaitwa Peter Michael Muganyizi.

Aliendelea kuwa alimchukua wakaenda chumba kingine kwa ajili ya kumchukua maelezo na kwamba, alikuwa na kovu na bandeji usoni.

Shahidi huyo alidai baada ya kufika chumbani alimweleza mtuhumiwa haki zake ikiwamo kuwa anaweza kuwa na wakili wake, au ndugu au rafiki wakati anamchukua maelezo, lakini alimweleza hakuna haja na nilianza kuandika maelezo yake kuanzia saa 2:40 asubuhi hadi saa sita mchana.

Alidai kisha alimpa maelezo hayo ayasome na kukubali kuwa ndiyo yenyewe na akasaini.

Wakili Kidando aliiomba mahakama imruhusu shahidi ayatambue maelezo hayo na alipewa kisha akasema ni yenyewe na yupo tayari kuyatumia mahakamni kama ushahidi.

Shahidi huyo alianza kusoma maelezo hayo kuwa Muganyizi alizaliwa Kyaka mkoani Kagera, mtoto wa pili kwao kuzaliwa, baba yake alishafariki na mama yake anaishi Kayanga Karagwe mkoani humo.

Maelezo yasomwa

“Mwaka 2010 nilifika Mwanza nikitokea Ngara, nilifikia kwa rafiki yangu Ally maeneo ya Mirongo, katika kutafuta maisha tulienda Sirari kufanya biashara huko tulikutana na Paul mkubwa na Paul mdogo, wakatuambia twende Kenya kwa Omuga.

“Tukiwa Kenya tulipora bunduki ya shortgun na risasi tisa, ila tulimtoroka Omuga tukaja Mwanza, tulipofika maeneo ya Isangijo tulikamatwa mimi nilikuwa nimebeba zile risasi tisa na mwenzangu bunduki, tulifungwa kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha.

“Julai 2012 tulitoka gerezani, nikiwa mtaani (Mwanza) nilikutana na Chacha (mshtakiwa wa pili) na tulifahamiana kutokana na kazi za kupora na tukawa tunapanga mikakati.

“Oktoba 11, 2012 mchana nilipokea simu ya Chacha akisema tukutane kesho (Oktoba 12) maeneo ya Nyashana jeshini ili tupange kazi ya kufanya, kweli tulikutana akasema tutafute hela za kwenda Dar es Salaam na tukapanga twende tukapore Kiseke, Kilimahewa na huko Nyamanoro.

“Tulipanga tukutane saa 2:00 usiku Shule ya Msingi Mbugani Nyakabungo, tulikutana watu watano kati ya hao mmoja alikuwa amebeba mfuko uliokuwa na bunduki tukapanga sasa twende huko tukavamie.

“Tulipita Thaqaaf, Mji mwema tukatokea mnada wa Kilimahewa, tulipofika hapo mwenye begi alimpa Chacha ile silaha tukaanza kujiandaa kwa ajili ya kazi.

“Tulipofika Lumala tulivamia Grocery tukachukua simu tano, tukaenda Kiseke tukakutana na mama anashuka kwenye daladala tukampora simu moja alisema hana kitu kingine, tukapita Lumala tukakuta kiduka kipo wazi tukachukua simu na hela, tukapita Nyamanoro kwa Mama Mzungu Mhaya tukachukua simu nne, kisha tulienda kukaa karibu na makaburi ya Kitangiri ili tuone tumepata nini.

“Tulipata simu 14 na Sh300,000 kati ya hizo nilipata Sh50,000, Ilibidi tuondoke hapo tulikubaliana tupite Kitangiri ili turudi Isamilo.

“Wakati tunaenda barabara ya Kitangiri inayokwenda Bwiru, tuliona gari imewasha taa, tukaikimbilia tukisema hela hiyo, hela hiyo, tulipofika kwenye gari hiyo tukakuta mwanaume na mwanamke, tukawaambia sisi ni maaskari, yule mwanaume (Barlow) akauliza ninyi ni maaskari wa wapi, hamnijui kwamba mimi ni kamanda wa polisi?

“Chacha aliniamuru mpige risasi huyo, nilimpiga kwa kutumia silaha ya shortgun greener yenye namba 13002 ilikuwa imekatwa mtutu, najua kwa sababu nilipitia mgambo mwaka 1995.

“Nilizunguka upande wa yule mwanamke nikachukua simu halafu tuliondoka, kesho Chacha alileta simu saba tuziuze ili twende Dar es Salaam, niliuza moja aina ya LG, nilimuuzia Bahati kwa Sh25,000 lakini alinipa Sh20,000 nyingine ikabaki namdai, nilichukua namba yake ya simu tuwe tunawasiliana kwa ajili ya kunitumia hela hiyo iliyobaki.

“Tarehe 14/10/2012, Chacha aliniambia wenyewe wameenda Dar es Salaam nikasema nitakuja tarehe 15, hata hivyo nilienda tarehe 16 kwa kutumia lori hadi Singida, hapo nikapanda basi la kunileta Dar es Salaam.

“Tarehe 18 nilipigia simu na Chacha akasema nimkute Kariakoo, kweli tulikutana nikaenda naye Gongolamboto kwake, tarehe 19 akanihamishia kwenye gesti Vingunguti akasema tutafute silaha nyingine kwa ajili ya kuendesha maisha.

“Alisema kuna kampuni ya ulinzi wana silaha tulienda hapo tarehe 23 lakini akasema yeye hataweza kwenda kwa sababu wanamfahamu hivyo akatupa kijana Buganzi (mshtakiwa wa nne katika kesi hiyo), Chacha alitoa bunduki hiyo tuliyoitumia kumuua kamanda Mwanza tukaenda nayo ili tupore ile ya walinzi “Tulienda kwenye kampuni hiyo majira ya saa 4:00 usiku nikiwa mimi, Magige (mshtakiwa wa tatu) na Buganzi.

“Tulipofika pale (kampuni ya ulinzi) Magige alimvua mlinzi silaha begani kwa amri yangu kisha nikasema tuondoke, ghafla nilipigwa na kitu kizito kichwani nikadondosha bunduki niliyokuwa nayo (inayodaiwa kumuua Barlow), tulipofika mbele nilimwambia Magige anipe silaha aliyomnyang’anya mlinzi niijaribu kama inafanya kazi, nilipoijaribisha nilikuta inafanya kazi, tuliificha kwenye shimo njia ya kwenda Gongo la mboto.

Tukaenda gesti, majira ya saa 5:00 usiku nilisikia mlango unagongwa, nilipofungua alikuwa ni Chacha ameongozana na askari, wakatukamata na kutuleta kituoni.

Baada ya shahidi huyo kusoma maelezo hayo, alifuata shahidi wa 22, Mohamed Mtenda (42) ambaye ni mlinzi wa gesti hiyo inayojulikana kwa jina la Kaloreti ipo Vingunguti, Dar es Salaam, aliileza Mahakama walivyowekewa mtego na askari mpaka wakakamatwa Oktoba 24, 2012 majira ya usiku.

Shahidi huyo alidai mmoja wa watu hao waliokamatwa alikuwa amekaa kwa siku tatu na alikuwa akitoka ndani ya gesti kuanzia saa 2:00 usiku hadi saa 4:00 au alfajiri.

Alieleza kuwa Oktoba 23, 2012 aliingia saa 5:00 usiku walikwenda maofisa usalama wa kanda maalumu, wakajitambulisha kwamba wanataka kukagua chumba namba tano, aliwataka wampe hati ya ukaguzi, walipomuonyesha akawapeleka chumbani wakakuta mlango upo wazi, kuna viatu, begi la mteja mafuta na mswaki.

Kamanda Barlow aliuawa Oktoba 13, 2012 katika tukio lililotokea eneo la Kitangiri wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Washtakiwa katika shauri hilo ni Peter Muganyizi, Chacha Waikena, Magige Mwita, Buganzi Edward, Bhoke Marwa, Abdallah Petro na Abdalrahman Ismail. Kesi hiyo inaendelea leo.