KPMG yadhamiria kuzisaidia kampuni za kati kukua kiuchumi

Mkurugenzi wa kampuni ya KPMG Tanzania, Ketan Shah akiwa kwenye moja ya hafla za Top 100. Picha ya Maktaba

Muktasari:

  • Kwa kutambu umuhimu wa kukuza biashara, mkakati unaohitaji ushiriki wa wadau tofauti watakaofanikisha safari hiyo, kampuni ya KPMG inasema itaendelea kufanya hivyo ili kuongeza mchango wa sekta hiyo kwenye uchumi wa Taifa. Ushauri wa masuala ya fedha na mikakati ya kuendeleza biashara ni miongoni mwa maeneo ambayo washiriki wa mashindano ya Top 100 watanufaika nayo hivyo kuchangia kukuza miradi waliyonayo.

 

Kampuni ya kimataifa ya ukaguzi wa hesabu za fedha ya KPMG imesema itaendelea kuzisaidia kampuni za kati ili zikue kiuchumi na kufikia viwango vya kimataifa.

KPMG kwa kushirikiana na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ndiyo waandaaji wa shindano linalozihusu kampuni za kati lijulikanalo kama Top 100 ambalo hufanyika kila mwaka tangu 2011.

Shindano hilo huhusisha kampuni zenye mauzo ya kuanzia Sh1 bilioni hadi Sh20 bilioni kwa mwaka.

Lengo la shindano hilo ambalo mwaka huu linatarajiwa kufanyika Alhamisi ya Oktoba 25 ni kutengeneza kanzidata (Data base) ya kundi hilo ambalo kwa kiasi kikubwa limekuwa halitazamwi na wengi ili kuwasaidia kupambana na changamoto zinazowakabili.

Wadhamini wa shindano hilo ni Benki ya NMB ambayo ndiyo mdhamini mkuu na wengine ni Hoteli ya Hyatt Regency, Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na Azam TV.

Katika mahojiano na Gazeti la Mwananchi, mkurugenzi wa KPMG Tanzania, Ketan Shah alisema uamuzi wa kampuni hiyo kuwa sehemu ya waandaaji ulitokana na dhamira yao ya kutaka kuongeza ufanisi wa kampuni ndogo na za kati.

Alisema KPMG inazisaidia kampuni hizo ikiamini kuwa zina mchango mkubwa katika ujenzi wa uchumi wa Taifa na zinatoa ajira kwa watu wengi.

“Kwa ukubwa wao hawatuhitaji sisi katika shughuli zao kutokana na sababu mbalimbali licha ya kuwa milango yetu iko wazi kwa watu wote. Gharama zetu ziko juu, lakini hata vigezo vya kampuni kufanya kazi na sisi navyo ni sababu,” alisema Shah.

Pia, alisema licha ya KPMG kufanya kazi zaidi na kampuni kubwa na zile za kimataifa, inaamini katika kuzikuza kampuni changa kwa sababu zikikua zitakuza uchumi.

Shah alisema kampuni ikishiriki Top 100 inapata fursa ya kukua zaidi kwa kujua namna bora ya uendeshaji wa biashara, kujitangaza na kukutana na wafanyabiashara wapya hivyo, kupanua soko na kupata mawazo mbadala.

Alisema kampuni nyingi huwa hazifuati kanuni bora za uendeshaji wa biashara kuanzia kwenye menejimenti na utunzaji wa kumbukumbu za fedha.

“Kigezo kikubwa cha kushiriki (Top 100), lazima hesabu za fedha katika kampuni husika ziwe zimekaguliwa kwa miaka mitatu mfululizo.

“Kampuni zinazoshiriki hutangazwa bure katika magazeti ya MCL (waandaaji) na Kituo cha Televisheni cha Azam TV (wadhamini) lakini pia hukutanishwa na wadau wa huduma za kifedha kama NMB na DSE (wote wadhamini) hivyo kunakuwa na urahisi katika biashara zao,” alisema Shah.

Alisema fursa nyingine ambayo washiriki wa Top 100 wanapata ni kuhudhuria makongamano yanayoendeshwa na KPMG bila malipo.

Pia, Shah alisema wanaohitimu Klabu 101 hupata fursa ya kuchagua mada ya mihadhara inayoendeshwa na kampuni hiyo na kuhudhuria bila malipo. “Wengine wote wanapaswa kulipia,” alisema Shah.

Changamoto za uandaaji wa Top 100

Shah alisema changamoto kubwa iliyopo katika uandaaji wa shindano hilo ni namna ya kuwapata washiriki kwa kuwa wafanyabiashara wengi hawana taarifa kuhusu faida za kushiriki shindano hilo.

Changamoto nyingine alisema ni woga wa kuweka taarifa muhimu za kampuni kama kigezo cha ushiriki.

“Wafanyabiashara wengi wanaogopa kushiriki shindano hilo kwa kuhofia kuwa wataonekana wamepata faida kubwa, hivyo Mamlaka ya Mapato (TRA) itaanza kuhitaji kodi kubwa kutoka kwao jambo ambalo siyo la kweli na potofu,” alisema Shah.

Alifafanua kuwa kila kampuni inawajibika kulipa kodi na kufuata taratibu zote za uendeshaji wa kampuni husika kwa kuwa hapo ndipo wanaweza kujivunia ukuaji endelevu na halisi.

Vigezo vinavyotumika kuwapata washindi

Shah allisema kigezo kikubwa kinachoangaliwa ni ukuaji wa kampuni kwa asilimia na viashiria vingine vya ukuaji (KPI) kwa jumla.

“Hatuangalii ukuaji tu, faida, uharaka wa kampuni kulipa madeni yake kwa ufanisi na weledi wa watumishi wake kwa jumla.

“KPI zinazingatiwa zaidi, hivyo ni wito wangu kwa kampuni nyingi kushiriki zaidi kila nafasi inapotokea,” alisema Shah.