Kaborou: Kigoma tulikuwa wa kwanza kutimua wasaliti CCM

Muktasari:

  • Swali: Chama cha Mapinduzi kipo katika uchaguzi wake wa ndani, ni namna gani mnashughulika na wasaliti au mlishamalizana nao?

Wiki iliyopita tulifanya mahojiano maalumu na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma, Dk Amani Kaborou kuhusu mambo mbalimbali ndani na nje ya chama hicho, ambapo pamoja na mambo mengine anaeleza jinsi walivyopambana na usaliti ndani ya chama. Endelea.

Swali: Chama cha Mapinduzi kipo katika uchaguzi wake wa ndani, ni namna gani mnashughulika na wasaliti au mlishamalizana nao?

Jibu: Sisi Kigoma tulikuwa ni wa mwanzo mwanzo kabisa kuwaengua wale ambao wanasemekana wasaliti.

Swali: Mliondoa wangapi?

Jibu: hawakupungua hamsini (50).

Swali: Hawakubaki wengine?

Jibu: Uwezekano upo wakabaki wengine kwa sababu ni mapendekezo, na wengine walikuwa katika utaratibu wa kukata rufaa. Mnaweza mkamwondoa, akakata rufaa na akashinda.

Hapa kwetu Kigoma Mjini, kuna mmoja alikuwa mwenyekiti wa wanawake aliondolewa lakini alikata rufaa na chama kikamrudisha. Lakini walio wengi hawakurudishwa.

Swali: Ni aina gani ya usaliti waliokuwa wanatuhumiwa nao?

Jibu: Kwa kweli usaliti wa hapa ulikuwa ni kusaidia vyama vya upinzani.

Swali: Mlijiridhishaje kwamba kwenye waliwasaliti?

Jibu: Kwa kweli utaratibu huo hauanzii hapa. Unaanzia huko kwenye matawi na mashina wanakotoka.

Kule ndiko wanatafuta watu waliosaliti, wanakaa nao wanaona mienendo yao. Kule wanatoa taarifa kwenye kata na kata inapeleka kwenye wilaya na sisi huku tunaangalia vigezo vilivyotumika na kujiridhisha.

Kwenye Chama cha CCM huwezi tu ukamtuhumu mtu halafu ikawa imetosha. Hata mimi (mwenyekiti) nikimtuhumu, nitapeleka kwenye ya ngazi yake na kamati ya maadili ya huko itaangalia kama kweli amefanya hilo kosa.

Swali: Hao wasaliti walikuwa wanasaidia chama gani cha siasa?

Jibu: Ni ACT- Wazalendo. Hata mheshimiwa Rais (John) Magufuli si alisema bungeni siku moja, ‘we Zitto si ulipewa kura na CCM?’

Swali: Kwa hiyo kwa kumpigia kura ni kuisaliti CCM?

Jibu: Ehee ndiyo, kama umefanya wenzio wasishinde, ndiyo umewasaliti.

Swali: Kama ni hivyo basi wasaliti mliowachukulia hatua ni wachache, maana Zitto alipata kura kwa maelfu?

Jibu:, Hamsini ni wachache sana, ila tunaangalia kwenye mifumo. Kiongozi wa chama akisaliti chama anakuwa na ‘impact’ kubwa kuliko mwanachama wa kadaiwa. Hawa wa kawaida hawawajibiki kwa mtu yeyote, ila kiongozi ana vikao anavyowajibika kwavyo. Kwa hiyo hawa wengi walikuwa viongozi. Katika hali ya kawaida kiongozi akionekana kwenye mkutano wa upinzani, inakuwa rahisi kusema huyu kahamia, lakini wale wa kawaida wanasema ahaa, mimi nilikwenda tu kusikia.

Swali: Uchaguzi ndani ya chama umefikia wapi?

Jibu: Mpaka sana tuko katika ngazi ya kata. Ndiyo sasa tunakusanya mapendekezo ya wilaya, nadhani zote zimemaliza, maana jana tulipitia, Kibondo, Kakonko, Kasulu, Uvinza nao wameshamaliza. Kwa hiyo hivi sasa tunataka tujipange kutengeneza vikao vya mkoa kuanzia ngazi ya nidhamu, kamati ya siasa na baadaye halmashauri kuu ya mkoa ili kupitisha wagombea watakaokwenda kupigiwa kura. Tuko ndani ya muda, hatujachelewa hata kidogo.

Swali: Ni matatizo gani mnayokumbana nayo latika uchaguzi huo?

Jibu: Matatizo tunayokumbana nayo yanaweza kusemekana kuanzia uchaguzi huu. Maana uchaguzi huu umekataza kabisa watu kupanga safu, kwa maana ya kuteua watu ambao unajua baadaye watakuja kukupigia kura wewe katika awamu yako.

Kwa hiyo sasa kuna mahali ambapo watu au viongozi wa kata walikuwa bado hawajataka kuafiki. Na pale walipojaribu taka kuendeleza utaratibu huo, wananchi wamelalamika na kuwasilisha malalamiko yao ngazi za wilaya na wilaya nao wanatuletea ngazi ya mkoa.

“Hilo la kwanza la safu kwa kweli naona watu wengi walikuwa hawajaliafiki. Wanasema nini bwana, naona hilo limekuwa kila mahali tangu ngazi ya tawi na sasa kata.

Swali: Kupanga safu ni kufanya nini?

Jibu: Kwa mfano, kutoa fomu kwa watu wachache. Kwa sababu chama kingependa watu wengi wagombee, lakini unakuta katibu wa kata au wa wilaya au mtu mwingine

INAENDELEA UK26

Inatoka Uk25

anajaribu kuzificha, anataka watu wale ambao anafikiri watakuja kuunga mkono mlengo wake.

Swali: Vipi suala la kununulia watu kadi za uanachama?

Jibu: Hiyo nayo imekatazwa kabisa. Hilo pia ni kupanga safu. Unanunuliwa watu kadi na kuwalipia ada ili wakuchague, hapo umepanga safu.

Swali: Hili pia lilikuwapo?

Jibu: Huwezi kusema halikuwapo kabisa, hapana. Limekuwapo.

Swali: Mahali pengine watu wameshindwa kujitokeza kugombea, wanasema kwenye chama hakuna fedha, sasa wanabanwa na mengine, hapa hali ikoje?

Jibu: Hata hapa mwanzoni lilikuwapo, lakini baada ya elimu kutolewa wengi wamejitokeza na wamechukua fomu. Sisi hapa tuna ushindani mkubwa sana, kila nafasi inagombewa na watu wengi.

Mwanzo walisema kabisa ‘tulikuwa tunapangwa na viongozi’ na wanashangaa utaratibu wa uchaguzi safari hii kwamba mtu anajichukulia fomu mwenyewe.

Wanasema mbona uchaguzi safari hii ni tofauti kabisa, wanaruhusiwa kuchukua fomu kwa maana ya kwamba zamani hawakuwa wanachukua fomu, walikuwa tayari wanateuana na kuchukuliana.

Wakati mwingine hata kuchaguliwa walikuwa hawachaguliwi, hata uchaguzi hautangazwi. Yule aliyechukua fomu ndiyo anajaza na kuzirudisha. Lakini sasa ni tofauti, kuna mtu, siwezi kutaja hapa ni wapi maana sina takwimu kamili, alikuwa mgombea pekee lakini amepigiwa kura nyingi za hapana. Na kuna mwingine hapa kwenye Jumuiya amepata kura moja. Ebu fikiri katika mkutano wa watu karibu 40, unapata kura moja.

Swali: Wewe mwenyewe unagombea tena?

Jibu: Ndiyo nagombea

Swali: Nafasi gani?

Jibu: Hii hii ya mwenyekiti.

Swali: Umeshapanga safu yako?

Jibu: (Anacheka) Kwa sababu sina uzoefu wa kupanga safu, hili halinipi shida. Sina uzoefu wa kupanga safu. Kwani nilipoingia hapa nilikuwa na safu gani. Na sasa hivi wamejitokeza watu 12 kuwania uenyekiti.

Swali: Ulipogombea mara ya kwanza mlijitokeza wangapi?

Jibu: Utaratibu ulikuwa tofauti, kwa kweli mimi sikumbuki vizuri, lakini nadhani tulioteuliwa na Kamati Kuu tulikuwa wanne. Sasa kama kulikuwa na wengine walikuwa wameomba, hao siwakumbuki.

Swali: Utaratibu wa sasa ukoje?

Jibu: Sasa hivi tutapanga kwenye vikao vyetu na baadaye kamati kuu ndiyo itaamua wangapi warudi na kina nani.

Na sasa hivi utaratibu ni tofauti, siku majina yanarudi ndiyo siku hiyohiyo ya kupiga kura, hakuna muda wa kampeni.

Swali: Nini kama mkoa mnafanya shughuli gani na majina ya wagombea hao?

Jibu: Sisi tunapanga grade tu na kuiachia kamati kuu kwa uamuzi. Kwanza yatapitia kamati ya maadili, baadaye kamati ya siasa na halmashauri kuu ya mkoa.

Swali: Baadhi ya vikao vya kujadili majina wewe ndiyo mwenyekiti, utapitia pia jina lako?

Jibu: Hapana, hapo siongozi mimi anakaa katibu

Swali: ACT- Wazalendo ndiyo inaongoza halmashauri hapa na mbunge ni wa upinzani, mahusiano yenu kisiasa hapa yakoje?

Jibu: Hapa Kigoma upinzani kabla ya 2012 ulishashika mizizi kuliko mikoa mingine, tulipoingia sisi kwenye uongozi wa chama, na sisi tulikuwa kwenye upinzani, tunajua mbinu na hoja za kukiteteresha chama tawala.

Kwa hiyo tulifanya vikao vingi sana. Sijui kama kuna kata ambayo sijafika. Tumezungumza na tunazungumza kile ambacho tunaamini ndiyo ilikuwa mbinu ya wapinzani kuwarubuni au kuwakatisha tamaa wananchi. Mnapotoa zile mbinu na zile siri, wananchi wanasema, ‘ahaa, kumbe tulikuwa tunadanganywa sisi’.

Kazi ni kuwaambia tu ukweli. Hakuna mtu wa Kigoma wala Tanzania anayeweza kubisha kwamba Mkoa wa Kigoma ni wa mwisho kimaendeleo, tangu kipato cha wananchi, rasilimali na miundombinu ya maji, barabara na reli.

Unamuuliza mtu wa Kigoma kama kweli anapenda maendeleo yake au anapenda tu kusaidia chama. Kwa mfano, unapochagua NCCR-Mageuzi, mwenyekiti wake wakati ule (James Mbatia) amewekwa bungeni na mwenyekiti wa CCM.

Halafu unakuta chama hicho kina wabunge wanne mkoani Kigoma na hakina mbunge mwingine mahali popote Tanzania, unawauliza wale watu, hivi kuichagua NCCR ni kuhitaji maendeleo au kuisaidia tu NCCR, maana haina waziri, haina Serikali.

Swali: Kuna tatizo kuwa na wabunge wa upinzani?

Jibu: Hili wala siyo siri, hapa tulikuwa na wabunge watano wa upinzani na watatu wa CCM, hivyo ajenda ya watu wa Kigoma lazima ifikishwe bungeni na upinzani. Na katika mfumo huu wa siasa za vyama vingi katika maeneo yetu haya ya Afrika, kila mtu anapenda apeleke maendeleo kwao kwanza. Unawauliza, sasa hao wabunge wenu wa upinzani wanaweza kuwashawishi wabunge walio wengi wa CCM wapeleke maendeleo kwenye maeneo yenu?

Kwa hiyo unawaeleza kua mnakuwa mnacheza na kura zenu. Mnatakiwa mjiunge na chama chenye Serikali, kinachokusanya kodi nacho kijue kwamba nanyi ni sehemu yake. Kitu kama hicho ukiwaambia wananchi wanaona ni kweli.

Swali: Hizo ni kauli za kisiasa au ndiyo uhalisia?

Jibu: Ndiyo ‘reality’ (ukweli) ya siasa. Kama mtu yumo kwenye mfumo wa siasa za vyama vingi na haelewi hilo, basi inabidi akajifunze upya.

Swali: Kwa hiyo ndiyo Serikali ya kuyabagua maeneo yenye wabunge wa upinzani?

Jibu: Aha, siyo kwamba ni sera ya Serikali, Serikali inatakiwa ikawahudumie wananchi wote.

Na nadhani Magufuli ni shahidi wa kweli, kila anapopita anaweza maji, anaweka barabara na si kwamba watatu watu wa CCM peke yake, watatumia na wale wengine.

Lakini ukweli ni kwamba katika mfumo wa vyama vingi kama alivyokuwa anasema (Mizengo) Pinda, (waziri mkuu mstaafu), kwamba ‘hapa tuna kasungura, tunajua kabisa kwamba hata ungegawa kwa ufundi wa namna gani hakawezi kutosheleza, kwa hiyo wale wengi lazima wasaidiane wapate mnofu mkubwa zaidi.

Siyo kwa sababu Serikali yao imewaambia wasiweze kuwasaidia wenzao, ni kwa sababu wa ni wengi na wanataka warudi. Watahakikisha kule kwenye mwenzao watahakikisha angalau anapata. Ndivyo hali ilivyo.

Hivi unaweza ukaweka timu moja ina wachezaji sita na nyingine ina mchezaji kumi na mmoja 11 halafu unategemea hawa wachezaji sita watawafunga wale 11, inaweza lakini siyo mategemeo.