Thursday, August 9, 2018

Kalanga mgombea pekee CCMAliyekuwa mbunge wa Monduli, Julius Kalanga

Aliyekuwa mbunge wa Monduli, Julius Kalanga 

By Mussa Juma, Mwananchi Mjuma@mwananchi.co.tz

Arusha. Siku mbili baada ya kundi la wanaCCM kujitokeza hadharani kupinga aliyekuwa mbunge wa Monduli, Julius Kalanga kurejeshwa kugombea ubunge katika jimbo hilo, mwanasiasa huyo amechukua fomu ya kugombea akiwa mwanaCCM pekee.

Wiki mbili zilizopita, Kalanga alijiuzulu ubunge wa Monduli aliokuwa akiushikilia kwa tiketi ya Chadema.

Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula amekaririwa leo na MCL Digital akisema kuwa, wanaompinga Kalanga wanaonyesha hofu tu, lakini

Kamati Kuu ya CCM ndiyo itakayoamua nani awe mgombea wao katika kikao kitakachofanyika mwezi ujao.

Leo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Monduli, Wilson Lengima amesema hadi jana, siku ya mwisho ya kuchukua fomu za ubunge ni Kalanga pekee aliyekuwa amechukua.

"Taarifa nilizonazo ni kuwa amechukua fomu Kalanga pekee na kama kutakuwa na mabadiliko tutatoa taarifa," amesema.

Soma Zaidi:

Akizungumza na Mwananchi Digital, Kalanga pia amesema amechukua fomu kutetea wadhifa wake na kuwashukuru wanaCCM wenzake.

"Nimechukua fomu za ubunge na nawashukuru sana wanaCCM wenzangu kwa kuendelea kuniamini," amesema.

Mapema wiki hii wanaCCM zaidi ya 40 kutoka kata tatu kati ya 20 za Wilaya ya Monduli waliandamana kumpinga

Kalanga kugombea ubunge kupitia chama na kutuhumu kuwapo kwa njama za kutaka kumfanya mgombea pekee.

Hata hivyo, hadi jana jioni ikiwa ni siku ya mwisho ya kuchukua na kurejesha fomu ndani ya CCM, hakuna aliyempinga Kalanga.


-->