Kama unadhani ulemavu ni ugonjwa msikilize mshindi wa pili kidato cha sita (2)

Erick Mlasini akiwa annaongea na simu huku  ameshikilia gitaa.Picha na Shatron Sauwa

Muktasari:

Erick Mlasani, mtoto huyo wa kwanza katika familia ya wauguzi, Maximilian Mlasani na Lidya Katabazi yenye watoto wanne, alizaliwa Oktoba 28, 1996 akiwa hana tatizo lolote.

Dodoma. Jana tuliangalia jinsi Erick Mlasani, kijana aliyeshika nafasi ya pili kitaifa katika masomo ya sanaa akitokea Shule ya Sekondari Mvumi DCT, Dodoma alivyotimiza ndoto yake ya kufanya makubwa katika masomo yake licha ya hali ya ulemavu wa macho aliyonayo. Leo anasimulia jinsi alivyofikwa na ulemavu huo akiwa mwanafunzi wa darasa la saba. Endelea…
Erick Mlasani, mtoto huyo wa kwanza katika familia ya wauguzi, Maximilian Mlasani na Lidya Katabazi yenye watoto wanne, alizaliwa Oktoba 28, 1996 akiwa hana tatizo lolote.

Alianza masomo ya msingi katika Shule ya Biharamulo mwaka 2003 na akiwa darasa la saba mwaka 2009, ndipo alipofikwa na masaibu.

“Ilitokea tu ilikuwa usiku niko darasani mwalimu anafundisha tuition (masomo ya ziada), pembeni kuna wanafunzi alikuwa anawaadhibu na mimi mara nilihisi kama kijiti kimenipiga juu ya jicho (la kulia) ndio ilikuwa chanzo cha kutoona,” anasema.

Anasema siku iliyofuata kulikuwa na mtihani wa majaribio (mock) ambao alikwenda kuufanya kwa kutumia jicho moja baada ya jingine kupoteza uoni na baada ya siku mbili macho yote yalivimba.

Alikwenda hospitali ambako alipatiwa dawa za kuondoa uvimbe na wekundu uliokuwa katika macho yake na kuelezwa kwamba baadaye yatakuwa sawa.

“Uvimbe uliondoka lakini macho yote mawili yalipoteza uoni kabisa. Nimeacha kuona kabisa Novemba 18, 2009.

“Nilipelekwa Hospitali ya CCRBT nikapimwa vipimo vyote wao walikuwa hawaoni tatizo. Hata CT Scan ilionyesha sina tatizo lolote,” anasema Erick.
Anasema baada ya hapo alirudishwa nyumbani ambako alikaa kwa muda wa miezi mitatu kabla ya kupelekwa tena kwenye matibabu bila mafanikio.

Anasema ilipofika Oktoba 2010 aliwaeleza wazazi wake kuwa hawezi tena kukaa nyumbani bila kusoma, “nikasema siwezi kukaa tena bila kusoma, niende kusoma kama kuona nitaona hukohuko.

“Mungu atanigusa hukohuko. Hapo mzazi wangu akaanza kutafuta shule. Nikapata shule moja inaitwa Buigiri (Wilaya ya Chamwino, Dodoma),” anasema.

Taarifa za kushindwa kwake kufanya mitihani ya kumaliza darasa la saba zilikuwa zinafahamika serikalini, hivyo alipewa nafasi ya kufanya mitihani hiyo mwaka 2011.

Alipofika Buigiri alianza kwanza kujifunza maandishi ya nukta nundu kwa mwezi mmoja na baadaye akafanya mtihani wa shule na matokeo yake yaliwaridhirisha walimu wake kuwa ana uwezo wa kufanya mitihani ya Taifa ya darasa la saba.

“Nilichaguliwa kujiunga na shule hii. (Mvumi DCT), nikasoma hadi form four (kidato cha nne). Nilipata division one na kuchaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari ya Kisimiri mkoani Arusha lakini sikwenda nikaamua kubaki hapahapa (Mvumi),” anasema Erick.

Mtazamo chanya

Baadhi ya watu wanaofikwa na hali hiyo huipokea kwa mtazamo hasi, lakini Erick anasema anaiangalia katika mtazamo chanya hasa kwa jinsi alivyopambana kupata mafanikio.

“Nadhani ningekuwa mtu wa kawaida (anayeona) nisingeweza kufanya haya ya kuwa inspire (kuwavutia) watu wengi na kuwafanya kujua kumbe wanaweza.

“Kwa hiyo hii hali si kama ninaipenda, lakini imekuja kwa sababu ya kubadilisha maisha ya watu wengine,” anasema kijana huyo. Anasema kuna wazazi au walezi ambao wanawafungia ndani watu wenye ulemavu wakidhani kuwa hawawezi na ni mizigo katika familia zao, lakini kilichotokea kwake kimewaonyesha kuwa wanaweza kufanya maajabu.

“Wakisaidiwa na kupewa nafasi ya kusoma na shughuli nyingine wanaweza. Kwa hiyo nikiangalia katika mtazamo huo sioni kama hali yangu ni hasi, ninaona ni chanya na kuna matunda mengi ninayapata na itawabadilisha watu wawe na mtazamo mwingine wa maisha,” anasema.

Mama azungumza

Lidya Katabazi ambaye ni mama mzazi wa Erick anakumbuka siku za mwanzo baada ya mwanaye huyo kupata ulemavu.

Anasema maswali ambayo Erick alikuwa akimuuliza yalikuwa yakimuumiza na wakati mwingine kumfanya alie. “Ananiuliza mama mbio za sakafuni huishia ukingoni? Kwa maana kwamba alikuwa na nia ya kuendelea kusoma lakini sasa hali imekuwa hivyo. Alikuwa na maana kwamba hataendelea kusoma tena kutokana na kukaa nyumbani miaka miwili tukihangaika na matibabu yake,” anasema Lidya.

Anasema Erick alikuwa akipenda kusoma na kutokana na juhudi hizo, waliamua kutafuta mwalimu wa kumsaidia masomo ya ziada mara baada ya kutoka shuleni.

“Muda mwingine ukimtuma aende kukuletea kitu jikoni huinuka na kalamu. Yeye madaftari yalikuwa hayatoki mgongoni mwake, mpaka nikamwambia mwanangu hayo madaftari yatakufanya upinde mgongo lakini wapi,” anasema.

“Sasa lilivyoingia tatizo hili lilileta simanzi kubwa katika familia yetu. Lakini baadaye nikajiuliza kwa nini nisimtafutie shule? Ila sasa nikawa najiuliza atasomaje? Ataendaje haoni, lakini rohoni nilipata ujasiri kuwa ataweza kwa sababu Mungu atamsimamia katika safari yake ya masomo.”

Lidya anasema wakati huo baba yake Erick alikuwa masomoni Dodoma ndipo alipomweleza kuhusu kumtafutia shule na kupata ya Buigiri ambayo ni shule jumuishi.

Mama huyo anasema hawezi kumsahau aliyekuwa mwalimu mkuu wa shule hiyo akimtaja kwa jina moja la Hosea kwa ushauri wa kisaikolojia aliompa baada ya kumpeleka mtoto huyo. “Aliniambia nisiwe na tabu. Alijua ninafikiria jinsi mtoto atakavyomudu masomo yake bila msaada wake.

“Aliniambia baada ya wiki moja mwanangu Erick atakuwa ameshazoea mazingira na atakuwa akifanya kila shughuli mwenyewe kama wanavyofanya wanafunzi wengine,” anasema mzazi huyo.

Anasema kuna changamoto nyingi za kulea watoto wenye ulemavu lakini kwa msaada wa Mungu, amejikuta mambo yakienda sawa kwa maana ya kumwezesha Erick kufikia ndoto yake.

“Anapotoka kwenda kufanya vitu vyake katika mazingira ya nyumbani ni lazima awe na mtu ambaye anamsaidia, hawezi kwenda pekee yake,” anasema.

Lidya anawashauri wazazi wenye watoto wenye ulemavu wasiwafiche, bali wawajenge katika misingi ya kuwapa elimu.

“Kutoona si kwamba kunamfanya ashindwe kufanya shughuli zake. Tunapaswa kuwasaidia kwa kuwawezesha kupata elimu, leo upo kesho haupo itakuwaje? Kama Mungu atakuwa amekuita ukamuacha pekee yake nani atakuja kuifanya hiyo kazi kama hana elimu?”

Mbunge atia neno

Mbunge anayewakisha watu wenye ulemavu, Amina Mollel anampongeza Erick kwa mafanikio hayo akisema ameonyesha kuwa na ulemavu si kulemaa.