Friday, August 11, 2017

Kamati za Bunge kuanza Septemba 5

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kamati za Kudumu za Bunge zitaanza kukutana kuanzia Agosti 28 mwaka huu mjini Dodoma kutekeleza majukumu yake kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Nane wa Bunge uliopangwa kuanza Septemba 5.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Bunge leo Ijumaa imesema kuwa Spika Job Ndugai ameziita kamati hizo kuanza shughuli zake tarehe hiyo kwa mujibu wa Kanuni ya 117 ya Kanuni za Kudumu za Bunge. Imeeleza kuwa Spika ameziita Kamati ya Masuala ya ukimwi na Kamati ya Bajeti kukutana kuanzia Agosti 21, 2017.

 Katika kipindi chote hicho kamati katika utekelezaji wake kisekta zitapokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa majukumu ya wizara zinazosimamia kwa mujibu wa Kifungu cha 6 na kifungu cha 7 (1) (c) na (d) cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Bunge.

"Kamati ya Sheria Ndogo itachambua Sheria zilizowasilishwa mezani wakati wa Mkutano wa Saba wa Bunge ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Kifungu cha 11 cha nyongeza ya Nane ya Kanuni za Bunge.

Imeeleza Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) itachambua taarifa ya uwekezaji kwa mujibu wa Kifungu cha 12 cha nyongeza ya Nane ya Kanuni za Bunge.

Taarifa hiyo pia imeeleza Kamati ya Bajeti itakagua shughuli za Wizara ya Fedha na Mipango  kwa mujibu wa Kifungu cha 9 cha nyongeza ya Nane ya Kanuni za Bunge.

"Kamati zinazosimamia matumizi ya fedha za umma ambazo ni Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zitachambua taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka unaoishia tarehe 30 Juni, 2016."

-->