Kampuni za tumbaku zazuia mbegu

Muktasari:

Mwakilishi wa Kampuni ya TLTC Limited, Wilson Urio alisema wameshapeleka mbegu kwenye maeneo husika lakini hawajazisambaza baada ya kupata maelekezo kuwa wasizigawe hadi upatikane mwafaka wa bei.

Tabora. Kampuni za ununuzi wa tumbaku zimegoma kusambaza mbegu kwa wakulima kwa madai kuwa wastani wa bei msimu ujao ni mkubwa.

Mwakilishi wa Kampuni ya TLTC Limited, Wilson Urio alisema wameshapeleka mbegu kwenye maeneo husika lakini hawajazisambaza baada ya kupata maelekezo kuwa wasizigawe hadi upatikane mwafaka wa bei.

“Sisi tumepewa maelekezo tusigawe mbegu hadi suala la bei ya msimu ujao lipate ufumbuzi,” alisema Urio.

Wakitoa malalamiko kwa wajumbe wa Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB) iliyotembelea masoko hayo wilayani Urambo, wakulima wa zao hilo, walisema hadi sasa hawajapata mbegu wakati msimu tayari umeshaanza.

“Tunalima kwa kalenda ya mwaka ambayo kipindi hiki ni kupata mbegu ambazo hatujapata ingawa tunasikia tayari zimefika,” alisema Mwenyekiti wa Chama cha Msingi Nsanjo, Hamis Musa.

Makamu mwenyekiti wa bodi hiyo nchini, Said Nkumba alisema kampuni za ununuzi wa tumbaku zinapimana ubavu na Serikali na kwamba, bodi yake ina kikao mjini Tabora na itatoa tamko kuhusu suala hilo.